NA JOHN BUKUKU- ARUSHA
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, anaendelea na mikutano ya kampeni leo katika mikoa ya Arusha na Manyara, ambapo atazunguka Karatu na Hanang’ akinadi Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025-2030.
Katika ziara hiyo, Dkt. Samia anatarajiwa kueleza utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, akibainisha miradi mikubwa ya maendeleo iliyotekelezwa katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, maji, barabara, nishati na miundombinu ya usafiri.
Aidha, anatarajiwa kutoa msisitizo wa namna serikali ijayo itakavyoendeleza miradi hiyo pamoja na kuanzisha mipango mipya itakayowanufaisha wananchi wa maeneo hayo na taifa kwa ujumla.
Katika mikutano yake, Dkt. Samia pia atazungumzia dhamira ya CCM kuimarisha sekta za kilimo, utalii, viwanda na nishati, sambamba na kusikiliza kero na hoja za wananchi ili kuziweka katika utekelezaji wa awamu ijayo ya uongozi.
Wananchi wa Arusha, Karatu, Manyara na Hanang’ wanatarajiwa kujitokeza kwa wingi kumpokea na kumsikiliza, huku viongozi wa CCM katika ngazi za mikoa na wilaya wakihamasisha wananchi kuendelea kuiunga mkono ilani ya chama hicho kwa ajili ya maendeleo endelevu ya Taifa.