Tabora.
Mgombea wa Urais kupitia Chama cha NLD, Mhe. Doyo Hassan Doyo, amewasili mkoani Tabora akiendelea na kampeni zake za kuomba ridhaa ya wananchi katika uchaguzi mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akihutubia wakazi wa Tabora, Mhe. Doyo alisisitiza dhamira yake ya kuliongoza taifa kwa misingi ya Uzalendo na Uadilifu. Amesema endapo atachaguliwa, ataweka mkazo katika kurejesha maadili ya taifa kwa kushirikisha viongozi wa dini kama washauri wa karibu wa Rais.
Mhe. Doyo alisema atatumia viongozi wa dini katika kutatua changamoto za uzalendo, kupambana na ufisadi na kulinda maadili ya taifa. “Viongozi hao watakuwa jopo maalum la washauri wangu, watanikumbusha pale nitakapokwenda tofauti. Uadilifu na maadili huanza na kiongozi mkuu wa nchi, hivyo rais mwenyewe lazima ajengwe kiimani, na kwa uzalendo,” alisema Doyo.
Mhe. Doyo aliongeza kuwa viongozi wa dini wana nafasi muhimu katika jamii na wanaweza kusaidia kuhamasisha uwajibikaji miongoni mwa viongozi wa serikali, hivyo mchango wao hautaachwa nyuma katika uongozi wake.
Aidha, akihutubia wananchi katika Kata ya Chemchem, eneo la Soko la Kachoma, Mgombea huyo wa NLD alieleza sera za chama chake zinalenga kumkomboa Mtanzania kupitia uchumi jumuishi na wenye kuwanufaisha makundi yote. Aliahidi kuongeza mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kutoka asilimia 10 ya sasa hadi kufikia asilimia 40, mikopo ambayo itatolewa bila riba, kwa sharti la kurejeshwa kwa wakati ili wananchi wengine pia waweze kunufaika.
Kwa upande wake, Katibu wa Kigoda cha Kina Mama Taifa wa NLD, Bi. Khadija Tambwe, aliwahimiza wananchi wa Tabora kutafakari historia yao na kuchagua mabadiliko.
“Ni zaidi ya miaka 60 tumeshuhudia ahadi zilezile kutoka chama tawala huku Tabora ikiendelea kubaki nyuma. Ni wakati sasa wa kumpa nafasi Mhe. Doyo na viongozi wa NLD ili kuona mabadiliko ya kweli,” alisema Tambwe.
Baada ya mkutano huo wa Tabora, msafara wa kampeni wa Chama cha NLD unaelekea mkoani Singida, Kondoa na kisha Dodoma, kuendelea na ratiba ya mikutano ya kampeni.