NA JOHN BUKUKU-ARUSHA
Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametangaza kupokea na kuanza kufanyia kazi maombi ya wadau wa utalii mkoani Arusha, ikiwemo ujenzi wa Kituo cha Taarifa za Utalii pamoja na barabara za katikati ya Jiji la Arusha.
Akihutubia mkutano wa kampeni kwenye Viwanja vya Michezo vya Sheikh Amri Abeid, Dkt. Samia amesema lengo kuu la serikali yake endapo atapewa ridhaa ni kukuza sekta ya utalii kwa kuongeza idadi ya watalii wanaofika nchini kufikia milioni nane katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
“Tutahakikisha wadau wa utalii wanapata huduma za kisasa ikiwemo Kituo cha Taarifa za Utalii na barabara nzuri katikati ya Jiji la Arusha. Hii itaimarisha taswira ya Tanzania na kuongeza idadi ya watalii,” amesema Dkt. Samia.
Amesisitiza pia umuhimu wa kuhamasisha na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza katika sekta ya makazi hususan hoteli mkoani Arusha, ili kuwapa watalii uhakika wa kupata huduma za malazi zilizo salama na zenye hadhi ya kimataifa.
Aidha, akizungumzia miradi ya miundombinu, Dkt. Samia amewahakikishia wananchi kuwa serikali yake itatekeleza mradi wa reli ya kisasa ya SGR yenye urefu wa kilomita 1,108 kutoka Bandari ya Tanga kupitia Arusha hadi Musoma, akisema Arusha itanufaika moja kwa moja na reli hiyo kupitia ajira na biashara zitakazochochewa na uwepo wa kituo kikubwa cha reli mkoani humo.
Katika hotuba hiyo, Dkt. Samia amegusia pia miradi ya viwanda, akitangaza kukamilika kwa taratibu zote za ujenzi wa Kiwanda cha Magadi Soda wilayani Monduli, akisema hatua inayofuata ni kuanza rasmi kwa ujenzi wa kiwanda hicho kitakachotoa fursa mpya za ajira kwa vijana wa mkoa wa Arusha.