NA JOHN BUKUKU- ARUSHA
Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kujenga Kijiji cha AFCON jijini Arusha ikiwa atapewa ridhaa ya kuunda serikali katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Akizungumza leo Oktoba 2, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha, Dkt. Samia alisema ujenzi wa kijiji hicho ni sehemu ya maandalizi ya Tanzania kushirikiana na nchi nyingine kuandaa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027.
Alibainisha kuwa kijiji hicho kitakuwa na miundombinu ya kisasa itakayowezesha timu shiriki kufanyia maandalizi, kufanikisha kambi na kutoa huduma za michezo kwa viwango vya kimataifa.
“Tunataka Arusha isiwe tu kitovu cha utalii bali pia kitovu cha michezo ya kimataifa. Kupitia Kijiji cha AFCON, tutajenga mazingira bora kwa vijana, kukuza michezo, kuongeza ajira na kuimarisha hadhi ya Tanzania katika ramani ya michezo ya Afrika na duniani,” alisema Dkt. Samia.
Aidha, Dkt. Samia alibainisha kuwa ujenzi wa kijiji hicho utafungua fursa mpya za kiuchumi ikiwemo uwekezaji, huduma za hoteli, biashara na kukuza pato la taifa kupitia sekta ya michezo na utalii.
Alitoa wito kwa wananchi wa Arusha na mikoa jirani kuendelea kuiamini CCM, akisisitiza kuwa chama hicho na serikali yake kimeonyesha uthubutu wa kusimamia miradi mikubwa ya kitaifa na kimataifa, ukiwemo mradi wa maandalizi ya AFCON 2027.