NA JOHN BUKUKU- ARUSHA
Mwanasiasa mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Makamu Mwenyekiti mstaafu, Kanali Abdulrahman Kinana, amesema kuwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM imetekelezwa kwa asilimia 98, ambapo ahadi za mgombea urais Dkt. Samia Suluhu Hassan zimekamilika kwa ufanisi katika sekta mbalimbali.
Amesema kuwa Dkt. Samia, kama mrithi wa uongozi wa taifa, ametekeleza kwa asilimia 100 ahadi alizotoa kwa wananchi wakati wa kampeni, jambo linaloonyesha dhamira ya chama na serikali yake kutambua wajibu walionao kwa Watanzania.
Kanali Abdulrahman Kinana ameyasema hayo wakati akizungumza Oktoba 2, 2025 katika muendelezo wa kampeni za Chama hicho kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Aidha amebainisha kuwa kila ahadi iliyotolewa na mgombea huyo imekamilika katika kila sekta, na kwamba viongozi wengine waliotangulia akiwemo Profesa Kitila Mkumbo tayari wameeleza kwa undani mafanikio hayo.
Kanali Kinana amesema kuwa tangu uhuru, chama hicho kimekuwa na misingi imara ya kauli mbiu zilizosisitiza kazi, ikiwemo “Uhuru na Kazi” na baadaye “Uhuru ni Kazi,” na kwamba kampeni ya sasa inayoongozwa na Dkt. Samia imekuja na kauli mbiu mpya ya “Kazi na Utu.”
Amesema kuwa maana ya kauli mbiu hiyo ni kwamba CCM na serikali yake wanatambua thamani na umuhimu wa kazi ili taifa liweze kuendelea kwa mshikamano na wananchi wote.
Aidha amebainisha kuwa kwa kipindi cha kampeni, mgombea huyo amezunguka zaidi ya nusu ya nchi akieleza utekelezaji wa ilani na kutoa matumaini mapya kwa Watanzania, sambamba na kusikiliza matatizo na hoja zao.
Aidha, Kanali Kinana amesema kuwa msingi wa utu ni haki, na moja ya haki muhimu kwa wananchi ni kushiriki uchaguzi. Ameeleza kuwa kupitia Tume iliyoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu, Jaji Othman Chande, wananchi maelfu wametoa maoni yao kuhusu haki na mapendekezo 333 yameandaliwa yakihusu wizara 23 na taasisi 47 za serikali, ikiwemo Polisi, Magereza, TAKUKURU na Mahakama.
Aidha amebainisha kuwa serikali inasimamia utekelezaji wa mapendekezo hayo 335 ili kuhakikisha haki za wananchi zinalindwa na kuimarishwa.
Kanali Kinana amesema kuwa Dkt. Samia anafanya kazi kwa kujituma na kuwajali Watanzania kwa dhamana aliyopewa mbele ya wananchi na Mwenyezi Mungu.
Aidha, amewaomba Watanzania kumpigia kura mgombea urais wa CCM, wabunge na madiwani wa chama hicho, akibainisha kuwa kwa kazi kubwa iliyofanywa na Dkt. Samia na namna anavyojieleza, wananchi wana kila sababu ya kumpa tena ridhaa ya kuongoza katika kipindi kijacho.