Mgombea Urais wa ACT Wazalendo, Othman Masoud, ameahidi kuimarisha sekta ya uvuvi Zanzibar endapo atachaguliwa kuwa Rais katika uchaguzi mkuu ujao.
Akizungumza na wavuvi wa Shumba, Micheweni Pemba, Othman alisema Zanzibar imezungukwa na bahari yenye rasilimali nyingi, lakini wavuvi bado wanakabiliwa na changamoto za ukosefu wa meli na vifaa vya kisasa.
Alibainisha kuwa serikali yake itahakikisha wavuvi wanapatiwa meli na vifaa vya kisasa, kujengwa vituo vya baridi na masoko ya samaki Unguja na Pemba, pamoja na viwanda vya kusindika samaki ili kuongeza thamani ya mazao na ajira kwa vijana.
Othman alitolea mfano wa Seychelles akisema Zanzibar inaweza kunufaika zaidi na uvuvi wa bahari kuu na kuuza samaki katika masoko ya kimataifa. Alisisitiza kuwa sekta ya uvuvi inaweza kuwa nguzo ya uchumi sambamba na utalii.
Pia aliahidi kuwepo na boti maalum za uokozi kwa wavuvi wanaopatwa na ajali baharini, na kuhakikisha usalama wao unalindwa. Aidha, alisema serikali yake itaimarisha Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM) kwa vifaa vya kisasa ili kulinda rasilimali za bahari.
Akizungumzia changamoto za wavuvi, alisema serikali yake itahakikisha upatikanaji wa vifaa na msaada kwa usawa bila ubaguzi, huku wavuvi wakihimizwa kutumia fursa za mikopo na miundombinu bora ya kuhifadhi na kuuza samaki kwa bei nzuri.
Wavuvi walioshiriki mkutano huo walieleza matatizo wanayokabiliana nayo ikiwemo ukosefu wa meli za bahari kuu, masoko ya uhakika na miundombinu ya baridi, na kuomba serikali mpya iwatambue na kuwasaidia zaidi.