NA JOHN BUKUKU- MOSHI
Mbunge wa Viti Maalumu na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Bi. Ummy Nderiananga, amesema kuwa utekelezaji wa sera na miradi ya maendeleo iliyoanzishwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan imechangia kuinua maisha ya watu wenye ulemavu nchini, hali iliyowapa sababu ya kumuunga mkono katika uchaguzi wa Oktoba 29, 2025.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni za CCM uliofanyika Uwanja wa Mashujaa, Moshi, Oktoba 1,2025, Bi. Ummy Nderiananga amesema kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia akimshukuru kwa kutoa zaidi ya Shilingi Bilioni mbili na Milioni mia moja hamsini na tisa kusaidia Vyama vya wenye ulemavu nchini Tanzania.ambapo hadi sasa shilingi milioni 408 zimepokelewa.
Aidha, amebainisha kuwa kwa mara ya kwanza watu wenye ualbino wamepata msaada wa mafuta maalumu ya ngozi yenye thamani ya shilingi milioni 60, na kunufaisha watu 5,000.
Katika sekta ya elimu, Bi. Nderiananga amesema kuwa Rais Samia amejenga mabweni 188 kwa wanafunzi wenye ulemavu nchi nzima, ikiwemo bweni lenye thamani ya shilingi milioni 80 lililojengwa Moshi ,
“Umetuonesha utu Mheshimiwa Rais, utu unalipwa kwa wema, tutakulipa Oktoba 29,” amesema Bi. Nderiananga.
Aidha, amebainisha kuwa wanafunzi 691 wenye ulemavu wameanza kupata huduma ya kufundishwa majumbani, ambapo Kilimanjaro watoto 13 tayari wameshaanza kusoma kwa mfumo huo.
Aidha, amesema kuwa uteuzi wa viongozi kutoka makundi ya watu wenye ulemavu kushika nafasi mbalimbali serikalini ni uthibitisho kuwa serikali ya awamu ya sita haibagui bali inathamini kila Mtanzania.
Bi. Nderiananga amebainiaha kuwa Dkt. Samia ametoa msaada binafsi wa shilingi milioni 36.7 kwa ajili ya ununuzi wa kiwanja Dodoma kwa ajili ya kujenga ofisi ya vyama vya watu wenye ulemavu, huku ofisi za muda zikikabidhiwa jijini Dar es Salaam,
Aidha, amebainisha kuwa Dkt. Samia ametoa misaada ya shilingi bilioni 7.7 kusaidia waathirika wa maafa nchini na nchi jirani ikiwemo Malawi.
Pia, Amesema kuwa kwa heshima ya mchango huo, wananchi wa Kilimanjaro na Watanzania kwa ujumla wanapaswa kumpa kura za kishindo Dkt. Samia Suluhu Hassan ili aendelee kuongoza nchi.