NA DENIS MLOWE IRINGA
MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini kwa tiketi ya CCM, Fadhili Ngajilo ameahidi wananchi wa kata ya Mshindo kuwa endapo watamchagua kuwa Mbunge atahakikisha Mkoa wa Iringa unapata timu ya ligi Kuu.
Akizungumza mbele ya umati wa wananchi katika mkutano wa kampeni wa kata kwa kata katika kata ya Mshindo, Ngajilo alisema kuwa suala mkoa wa Iringa kukosa timu ya ligi kuu ni kitu ambacho hakiiungi mkono hivyo kwa kushirikiana na madiwani watakaochaguliwa kwa tiketi ya CCM atahakikisha suala la michezo katika jimbo la Iringa mjini chanzo cha ajira kwa vijana
Alisema kuwa Michezo kwa mkoa wa Iringa imesuasua kwa muda mrefu hivyo akichaguliwa atalivalia njuga ili timu ya ligi kuu iwepo kwani ana uzoefu katika michezo mbalimbali mkoani hapa.
Aliongeza kuwa kupitia mashindano mbalimbali aliyokwisha anzisha kama kombe la Ngajilo ambalo sasa ji Vunjabei Cup atahakikisha anashirikiana na madiwani wa kila kata kuweza kuzalisha ajira kwa vijana kupitia michezo.
Alisisitiza kuwa katika mashindano aliyokwisha anzisha yamezalisha wachezaji wakubwa ambao wanatamba katika ligi kuu akiwemo Clement Mzize na kuongeza kuwa sio mpira wa miguu tu atahakikisha michezo kama rede, draft mpira wa Pete, wavu inakuwa mkombozi kwa vijana na tunataka iringa iwe nguzo ya uchumi na utalii kupitia michezo.
Katika kampeni hizo Ngajilo alisema kuwa licha ya kukuza michezo ameweka wazi mkakati wa kuubadilisha mji wa Iringa na kuusogeza hatua kwa hatua kuwa jiji kamili, kwa kuimarisha huduma za kijamii, kuendeleza miundombinu na kuanzisha viwanda vya kimkakati.
Aidha Ngajilo aliwataka wananchi wa kata ya Mshindo kuhakikisha kwamba wanajitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura kwa wagombea wote wa CCM kwa kura za kishindo kwa rais Dkt Samia Suluhu Hassan na madiwani wa kata zote za Iringa Mjini.




