Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amewasili jijini Victoria Falls, Zimbabwe, kushiriki Mkutano wa 22 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika na Nordic, unaofanyika kuanzia tarehe 2 hadi 3 Oktoba, 2025.
Akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Victoria Falls Mhe. Waziri Kombo amepokelewa na Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Mhe. CP Suzan S. Kaganda, pamoja na viongozi wa ngazi ya juu kutoka Tanzania na Zimbabwe. Ziara yake inafanyika kufuatia mwaliko rasmi kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara za Kimataifa wa Jamhuri ya Zimbabwe, Mhe. Prof. Dkt. Amon Murwira.
Mkutano wa mwaka huu unaongozwa na kaulimbiu isemayo: “Innovation for Impact: Leveraging Technology and Collaboration for Future-Ready Societies” (Ubunifu kwa Matokeo: Kutumia Teknolojia na Ushirikiano kwa Jamii Zinazojitayarisha kwa Baadaye). Kaulimbiu hii inalenga kusisitiza umuhimu wa ubunifu, teknolojia na mshikamano wa kimataifa katika kujenga jamii imara kwa maendeleo ya baadaye.
Shughuli za siku ya kwanza zinajumuisha Kongamano la Biashara (Business Forum) linalokutanisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchi za Afrika na Nordic (Denmark, Finland, Iceland, Norway na Sweden), kwa lengo la kukuza fursa za biashara na uwekezaji baina ya pande hizo mbili.
Katika mkutano huo, Mhe. Waziri Kombo anatarajiwa kuwasilisha vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita katika nyanja za biashara, uwekezaji, elimu, teknolojia na maendeleo ya kijamii, sambamba na kuimarisha ushirikiano wa karibu kati ya Tanzania na nchi za Nordic.
Aidha, atafanya mazungumzo ya kidiplomasia na viongozi mbalimbali kutoka barani Afrika na nchi za Nordic, ikiwa ni sehemu ya jitihada endelevu za kuimarisha uhusiano wa Tanzania na nchi washirika na marafiki wa maendeleo