NA JOHN BUKUKU- MOSHI
Mgombea wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuufungua Mkoa wa Kilimanjaro kwa kujenga barabara za viwango vya lami, zege na changarawe ili kukuza uchumi na kuongeza biashara ya kimataifa kati ya Kanda ya Kaskazini na nchi jirani.
Akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika leo Jumatano, Oktoba 1, 2025, katika Viwanja vya Mashujaa, Moshi Mjini, Dkt. Samia alisema barabara ni chachu ya maendeleo ya wananchi na hivyo serikali yake imepanga kuhakikisha mkoa huo unapata miundombinu ya kisasa ya barabara.
Miongoni mwa barabara alizotangaza kujengwa ni barabara ya Holili–Tarakea yenye urefu wa kilomita 53, ambayo itakuza biashara kati ya Tanzania na Kenya sambamba na kupunguza msongamano wa malori katika barabara ya Mwika–Tarakea.
Vilevile, ameahidi kujenga barabara ya mchepuko ya Kae–Airport yenye urefu wa kilomita 31 kwa kiwango cha lami, kukamilisha ujenzi wa barabara ya Moshi International School–Kibosho Kati–Kwa Raphael yenye urefu wa kilomita 13, pamoja na barabara za ndani za Mji wa Moshi kupitia mradi wa uendelezaji miji Tanzania (TACTIC).
Aidha, Dkt. Samia alisema mpango wa serikali yake pia utahusisha ujenzi wa barabara kwenye Wilaya za Rombo na Moshi Vijijini, huku Wilaya ya Same ikitengewa barabara za lami na zege katika maeneo ya Milimani ili kurahisisha usafiri wakati wa misimu ya mvua.
Dkt. Samia alisisitiza kuwa hatua hizo ni sehemu ya dhamira yake ya kuhakikisha Mkoa wa Kilimanjaro unakuwa na mtandao bora wa barabara unaowaunganisha wananchi, kukuza uzalishaji na kuongeza fursa za biashara za ndani na za kimataifa.