Mbunge Mteule wa Viti Maalum watu wenye Ulemavu na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu). Bi. Ummy Nderiananga, amemuombea kura mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Mashujaa mjini Moshi, Oktoba 1, 2025.
Bi. Ummy Nderiananga amesema kuwa tangu Dkt. Samia aingie madarakani, watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) wamekuwa wakipata huduma za kupaka mafuta baada ya kutolewa fedha kwa ajili ya huduma hiyo, ambapo awamu ya kwanza ilitolewa shilingi milioni 60 na zaidi ya watu 4,500 wamenufaika.
Aidha, amebainisha kuwa utu wa Dkt. Samia umewafuta machozi watu wenye ulemavu kwa kuwateua na kuwapa wawakilishi katika uongozi wa serikali, akisisitiza kuwa serikali yake inamjali kila mtu na haibagui.
“Umetuonesha utu Mheshimiwa Rais, utu unalipwa kwa wema, tutakulipa Oktoba 29,” amesema Bi. Nderiananga.
Bi. Ummy Nderiananga amesema kuwa chini ya uongozi wa Dkt. Samia yamejengwa mabweni 188 nchi nzima kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu ili waweze kupata elimu.
Aidha, Amesema kuwa katika Wilaya ya Moshi, bweni moja limejengwa kwa gharama ya shilingi milioni 80.
“Mhe. Rais, hapa Moshi kuna bweni moja limejengwa kwa milioni 80, na ukajenga shule ya bweni kwa wanafunzi wenye ulemavu.
”
Niwaombe Watanzania, mtu anayetuonesha anajali, ikifika Oktoba tusimuache,” amesema.
Aidha, amebainisha kuwa kabla ya Dkt. Samia kuingia madarakani, watu wenye ulemavu hawakuwa na ofisi, lakini serikali yake imejenga ofisi zao makao makuu ya nchi Dodoma kwa gharama ya shilingi milioni 34.
Pia, Bi. Nderiananga amesema kuwa mkoa wa Kilimanjaro unapokumbwa na majanga wamekuwa wakimkimbilia Dkt. Samia ambaye amekuwa msaada mkubwa kwao.
Amebainisha kuwa mara kadhaa ametoa misaada, ambapo zaidi ya shilingi milioni 7 zimetolewa nchi nzima kwa ajili ya kukabiliana na maafa.
UMMY NDERIANANGA: DKT. SAMIA AMEWAFUTA MACHOZI WENYE ULEMAVU
