Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Singida, Mhe. Aysharose Mattembe, akikabidhi mifuko ya saruji kwa viongozi wa Wilaya ya Manyoni. Kutoka kushoto ni
Muonekano meza kuu.
Wazazi wa wanafunzi wa darasa la sita na la saba wa shule ya msingi Sayuni waliofika shuleni hapo kushuhudia makabidhiano ya mifuko ya saruji iliyotolewa na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Singida, Mhe. Aysharose Mattembe.
Wanafunzi wa darasa la sita na la saba wa Shule ya Msingi Sayuni, wakiwa katika picha ya pamoja Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Singida, Mhe. Aysharose Mattembe baada ya kutoa msaada huo.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Singida, Mhe. Aysharose Mattembe akizungumza na Wanafunzi wa darasa la sita na la saba wa Shule ya Msingi Sayuni.
Na Dotto Mwaibale, Singida
MBUNGE wa Viti Maalum wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe ametekeleza ahadi yake kwa kutoa mifuko 50 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya Shule ya Msingi Sayuni iliyopo Wilaya ya Manyoni mkoani Singida.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi Mattembe alisema saruji hiyo ameitoa ili kutimiza ahadi aliyoitoa mwaka jana alipoalikwa mgeni rasmi katika mahafali ya darasa la saba.
“Tumeahidi, Tumetekeleza na Tunaahidi tena Kuchapa Kazi Zaidi kwa Juhudi na Maarifa mwaka jana 2019 nilialikwa kuwa mgeni rasmi katika shule hiyo kwenye taarifa yao waliniambia wameanzisha ujenzi wa madarasa kwa lengo la kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani, nilivutiwa na jitihada wanazozifanya walimu na wazazi kwani kila mwaka shule hiyo imekuwa ikishika nafasi ya kwanza kiwilaya niliwaahidi kuwachangia mifuko 50 ya saruji na leo hii namshukuru sana Mungu nimeweza kutimiza ahadi yangu” alisema Mattembe.
Mattembe alitumia fursa hiyo kuwaomba wananchi kuendelea kumuunga mkono Mhe Rais Dkt.John Magufuli katika sekta ya elimu kwa kujitoa kuchangia miundombinu ya shule ili kutekeleza nia ya Rais ya kutoa elimu bure lakini pia wanafunzi wetu kuwa katika mazingira bora wakati wakiwa shuleni.
“Nimpongeze Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sayuni, Stanley Jumamosi pamoja na walimu na wazazi kwa ushirikiano uliopo baina yao ambao umeonesha matunda hayo ya ufaulu wa wanafunzi” alisema Mattembe.
Katika hafla ya kukabidhi msaada huo Mattembe aliambatana na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Sayuni, Marios,
Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Manyoni, Ally Omary, Katibu wa Umoja wa Vijana Wambura Igeby, Katibu Mwenezi wa Kata ya Manyoni ambaye pia Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa vyumba vya madarasa Shule ya Msingi Sayuni, Lukas Boyboy, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Manyoni Jumanne Makanda, Mwenyekiti wa Jumuiya ya UWT Wilaya ya Manyoni Blandina Mawala, Katibu Msaidizi wa Chama Wilaya ya Manyoni Mwasiti Hamisi, Katibu wa UWT Wilaya ya Manyoni Mwadawa Ally na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, ndugu Fusi Charles.