Home Makala UPEKEE WA RAIS MAGUFULI

UPEKEE WA RAIS MAGUFULI

0
………………………………………………………………………………
Na Emmanuel J. Shilatu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli anasifikia kuwa na sifa kuu 3 ambazo ni Uzalendo, Uadilifu na Uchapa kazi. Nje ya utambuzi huo Rais Magufuli amejipambanua kuwa ni Kiongozi mwenye maono, utashi wa kisiasa na uthubutu wa hali ya juu unaomfanya aweze kukwamua yaliyoshindikana na aweze kuweka historia isiyofutika kwa Taifa kwa vizazi na vizazi.
Twende pamoja utaelewa nachokisema. Suala la Serikali kuhamia Dodoma lilikuwapo tangu mwaka 1973 lakini limeshindikana kutekelezeka kwa zaidi ya awamu 4 (zaidi ya miaka 40) lakini leo hii ndani ya miaka 4 tu Serikali nzima imehamia Dodoma.
Kwa zaidi ya miaka 40 ujenzi wa umeme Mto Rufiji ulikwama lakini leo hii ndani ya miaka 4 ujenzi umeanza ambao utazalisha megawatts zaidi ya 2115 ambao ni umeme mkubwa zaidi kuliko uliopo sasa. 
Tangu Dunia iumbwe Tanzania tunatumia treni ya Dizeli lakini leo hii ndani ya miaka 4 ujenzi wa reli ya kisasa kwa kiwango cha SGR unaendelea kwa kasi kuanzia Dar es salaam hadi Morogoro hadi Dodoma malengo yafike Mwanza na Kigoma. Utakuwa usafiri wa haraka, nafuu na unaobeba mizigo mingi. Hakika Rais Magufuli ni Kiongozi mwenye maono makubwa.
Kwa zaidi ya miaka 50 leo hii Watanzania tunashuhudia Wazungu wakinyenyekea madini yetu. Leo hii Serikali inamiliki asilimia 16 ya hisa katika makampuni ya uchimbaji madini, Serikali inapata gawio ka faida ya madini ya asilimia 50 kwa 50. Ni uzalendo, uadilifu na uthubutu wa Rais Magufuli umeleta manufaa haya.
Usafiri wa Treni kuelekea njia ya Dar – Dodoma – Kigoma ulikuwa unasuasua kwa zaidi ya miaka 15 leo hii imebaki historia, usafiri umeimarika.
Ni kama ambavyo usafiri wa Dar – Tanga – Arusha ulivyokufa kwa zaidi ya miaka 30 leo hii umeanza kufanya kazi ndani ya miaka 4 tu na kurejesha tabasamu na tumaini kwa Watanzania.
Kazi inaendelea, Treni ya abiria ya majaribio imewasili jijini Arusha  Februari 26, 2020, ikiwa ni mara ya kwanza tangu zaidi ya miaka 30 iliyopita zilipositishwa huduma za treni katika njia hiyo.
Kuna Mwananchi toka mkoa wa Mara ameniambia leo  Hospitali ya Rufaa mkoani Mara ambayo ujenzi wake ulianzishwa na Hayati Baba wa Taifa Mwl. J.K Nyerere lakini ilishindikana kujengwa kwa zaidi ya miaka 30 sawa miongo 3. Sasa ndani ya miaka 4 tu Mhe. Rais Magufuli kashafikia 99% ya ujenzi wa Hospitali hii. Kweli huyu kafufua ndoto za Mwl Nyerere na kuziendeleza.
Hayo ni kwa uchache sana kati ya mengi makubwa. Nyakati zote tumeshuhudia maono, utashi, uthubutu, uadilifu, uzalendo na uchapa kazi wa Rais Magufuli. 
Sisi Watanzania tuna jukumu la kufanya kazi kwa bidii na kuzidisha umoja imara kati yetu. Umoja wetu ni nguzo yetu.