Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi wa Mwanga katika muendelezo wa Kampeni za Uchaguzi kwa CCM mkoani Kilimanjaro tarehe 30 Septemba, 2025.
…………
NA JOHN BUKUKU – SAME, KILIMANJARO
Dkt. Samia amesema kuwa katika sekta ya maji, amefanikisha kutimiza miradi yote miwili ya maji iliyokuwa imeanzishwa na Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania, Hayati Alibabu Msuya. Aidha, amebainisha kuwa upatikanaji wa maji umeongezeka kutoka asilimia 77.5 kwa mwaka 2022/23 hadi asilimia 81.9 kwa mwaka 2024/25.
Dkt. Samia amesema hayo Septemba 30, 2025, katika muendelezo wa kampeni za Chama hicho, wakati akizungumza na wananchi na wakazi wa Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro.
Aidha, ameeleza kuwa Awamu ya Pili itahusisha kusogeza huduma ya maji kwa vijiji vilivyobaki, akitaja maeneo ya Same na Korogwe, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa kwa aliyekuwa Waziri Mkuu mstaafu, Hayati Alibabu Msuya, sambamba na ujenzi wa Barabara ya Msuya.
Amesema kuwa katika Wilaya ya Mwanga, serikali ya CCM imejenga minara sita ya mawasiliano ili kuimarisha huduma za simu na kuwawezesha wananchi kufanya shughuli za kiuchumi kwa ufanisi.
Pia, ameeleza kuwa katika sekta ya kukuza utalii, serikali imefungua lango katika Tarafa ya Mwanga kwa lengo la kuongeza idadi ya watalii.
Dkt. Samia amesema: “Niwapongeze Wana Mwanga maana ni wakulima wazuri,” na ameahidi kujenga soko kwa wananchi wa Mwanga, huku akibainisha kuwa soko kubwa litajengwa katika eneo la Chita.
Aidha, ameeleza kuwa serikali itaongeza nguvu ya kuzuia wanyama waharibifu kwa kujenga vituo vya ulinzi na kudhibiti uharibifu huo, sambamba na kuweka vitendea kazi vyote vitakavyosaidia kuwadhibiti wanyama hao.
Pia, ameeleza kuwa serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuondoa changamoto ya magugu katika Ziwa Ike, ili kuepusha athari kwa shughuli za uvuvi.
Dkt. Samia ametoa wito kwa wananchi na wakazi wa Mwanga kuichagua CCM ili iendelee kuleta maendeleo nchini na kwa Wanamwanga kwa ujumla. Amesisitiza kuwa wakikipa ridhaa Chama hicho, kitaleta heshima na ustawi kwa Wanamwanga na Watanzania wote.
Aidha, ameeleza kuwa katika sekta ya afya, serikali ya CCM imefanya kazi kubwa ya kusogeza huduma karibu na vijiji vyote vya Tanzania.