NA JOHN BUKUKU – PANGANI, TANGA
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kukamilisha ujenzi wa daraja la Pangani na barabara ya Bagamoyo–Saadani–Pangani–Tanga, akisisitiza kuwa miradi hiyo ni ya kimkakati kwa kufungua ukanda wa kaskazini kiuchumi na kuongeza fursa za kitalii na biashara.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika wilayani Pangani, Septemba 29, 2025, Dkt. Samia alisema ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 50 umefikia asilimia 75 na serikali imejipanga kuhakikisha inakamilika kwa wakati. Aliongeza kuwa daraja la Pangani litakapoanza kutumika litaondoa changamoto ya usafiri wa kusafiri umbali mrefu na kuunganisha kwa urahisi mikoa ya Pwani, Tanga na Kilimanjaro.
“Daraja la Pangani ni mkombozi wa wananchi na barabara hii ndiyo kiunganishi muhimu cha ukanda huu. Tukiimaliza, changamoto za usafiri zitakuwa historia,” alisema Dkt. Samia huku akihimiza wananchi kumpa kura ya ndiyo CCM katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, ili chama hicho kiendelee kusukuma mbele ajenda ya maendeleo.