Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC) , Bi. Khadija Ngasongwa na Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Ushindani wa Haki Zanzibar (ZFCC) Bi. Aliyah Juma wakisaini mkataba wa ushirikiano wenye lengo la kuimarisha ushindani wa haki sokoni na kulinda haki za walaji ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika hafla fupi iliyofanyika leo Septemba 29, 2025 jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Tanzania Bara, Dkt. Hashil Abdalah akizungumza katika hafla fupi ya kusaini mkataba wa ushirikiano kati ya FCC na ZFCC iliyofanyika eo Septemba 29, 2025 jijini Dar es Salaam.
…….
NA FRANCISCO PETER, DAR ES SALAAM
Tume ya Ushindani (FCC) na Tume ya Ushindani wa Haki Zanzibar (ZFCC) zimetiliana saini mkataba wa ushirikiano wenye lengo la kuimarisha ushindani wa haki sokoni na kulinda haki za walaji ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza leo Septemba 29, 2025 jijini Dar es Salaam katika hafla ya utiaji saini, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Tanzania Bara, Dkt. Hashil Abdalah, amesema kuwa makubaliano hayo yameweka misingi muhimu ya ushirikiano ambayo inahitaji utekelezaji makini kutoka pande zote mbili.
Amesema kuwa hatua ya kwanza ni kuteua watu au timu mahsusi zitakazosimamia utekelezaji wa makubaliano hayo. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuandaa mpango kazi au ramani ya utekelezaji (roadmap) ndani ya kipindi kisichozidi miezi mitatu ili kuhakikisha utekelezaji unaongozwa kwa mwelekeo ulio wazi.
“Tunahitaji kupanga muda mahsusi kwa kila jukumu ili kuhakikisha utekelezaji unafanyika kwa wakati. Bila ratiba ya utekelezaji, malengo hayawezi kufikiwa kwa ufanisi,” amesema Dkt. Hashil.
Amesisitiza hitaji la kuwajengea uwezo watumishi wa FCC na ZFCC kupitia mafunzo na semina elekezi, ili wawe na uelewa wa pamoja kuhusu malengo ya ushirikiano huo.
Ameongeza kuwa hatua hii ni sehemu ya utekelezaji wa maono ya viongozi wakuu wa nchi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi wanaotilia mkazo mazingira bora ya biashara na ukuaji wa sekta ya viwanda.
Aidha, ameelekeza kuwekwa kwa utaratibu wa kufanya tathmini ya utekelezaji, angalau kila baada ya miezi mitatu au sita, ili kupima maendeleo na kubaini maeneo yanayohitaji maboresho.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Bi. Khadija Ngasongwa, amesema kusainiwa kwa mkataba huo ni ushahidi wa mshikamano wa kitasisi na dhamira ya pamoja ya kuhakikisha masoko yanakuwa ya haki na yanayolinda walaji kote nchini.
“Ushirikiano huu unalenga kuongeza nguvu ya pamoja katika kukabiliana na changamoto kama vile ushindani usio wa haki na ukiukwaji wa haki za walaji, hali ambayo inaathiri pande zote za Muungano,” amesema Bi. Ngasongwa.
Amefafanua kuwa utekelezaji wa makubaliano hayo utajumuisha kubadilishana taarifa muhimu, kushirikiana katika mafunzo na tafiti, pamoja na kuboresha ufanisi katika utekelezaji wa sheria za ushindani na ulinzi wa walaji.
Bi. Ngasongwa amewataka wadau wa sekta husika kuchangamkia fursa hii ya ushirikiano ili kuimarisha utendaji wa pamoja na kuhakikisha mazingira ya biashara yanabakia kuwa tulivu na shindani.
Naye, Kaimu Mkurugenzi wa ZFCC, Bi. Aliyah Juma, ameseman kuwa taasisi yake iko tayari kushirikiana kwa karibu na FCC katika kutekeleza kikamilifu vipengele vya makubaliano hayo.
“Tumejipanga kushughulikia changamoto zote zinazokwamisha ushindani wa haki, kwa kushirikiana kwa karibu na wenzetu wa FCC. Tutaendelea kuwa bega kwa bega kuhakikisha malengo ya mkataba huu yanatimia kwa weledi,” amessma Bi. Aliyah.