NA JOHN BUKUKU – PWANI
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewahimiza Watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba 29, mwaka huu.
Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni mkoani Pwani, Dkt. Samia alisema hana shaka kuwa Watanzania hawatakuwa na sababu ya kutokipigia kura Chama Cha Mapinduzi kutokana na kazi kubwa za maendeleo zilizotekelezwa katika kipindi chake cha uongozi.
” Sioni sababu mwanapwani yeyote asiwe na furaha na hamu ya kukichagua Chama Cha Mapinduzi CCM, Kwa hiyo niwaombe Sana tarehe 29, Oktoba 2025 sote kwa pamoja na hapa na kauli mbiu ya ‘Twende Pamoja’ kwa hiyo utakapoamka pita kwa jirani yako kama ni balozi pitia watu wako wore kwa pamoja mwende mkakipigie kura Chama Cha Mapinduzi bila hofu yoyote tukachague CCM kwa. maendeleo, ” amesema Dkt. Samia
Amesema kazi kubwa ya maendeleo tumefanya, miradi ya barabara, afya, elimu, nishati na miundombinu ya usafirishaji na mingine inaendelea kutekelezwa. Nawaomba Watanzania wenzangu, twende kwa pamoja tukapige kura, twende tukachague CCM, kwa sababu tunaenda kuchagua maendeleo.
Ameongeza kuwa CCM kimeonesha uthubutu na dhamira ya dhati ya kuwaletea wananchi maisha bora kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati na huduma za kijamii zinazogusa maisha ya kila Mtanzania.
Dkt. Samia amehitimisha kwa kuwataka wananchi wa Pwani na Watanzania kwa ujumla kuonesha mshikamano wao kwa kujitokeza kwa wingi Oktoba ili kukihakikishia CCM ushindi wa kishindo na kuendeleza safari ya maendeleo ya Taifa.
Dkt. Samia Leo anaanza kampeni zake mkoani Tanga akinadi ilani ya uchaguzi ya 2030 huku akiwaelezea wananchi utekelezaji wa ilani ya 2025 na kazi zilizofanyika ambapo atakuwa na mikutano midogo ya wilaya za Pangani, Muheza na baadaye mkutano mkubwa wa kampeni utakaofanyika Tanga mjini.



