Mgombea nafasi ya Ubunge katika Jimbo la Peramiho kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bi. Jenista Mhagama amesema atawashangaa wananchi wa jimbo la Peramiho wakataowapigia kura vyama vya upinzani huku akisema kuwa CCM ndio chama pekee chenye kujua changamoto za wananchi na tayari imeshaonyesha dira ya kuleta maendeleo kwa wananchi wa Songea Vijijini.
Bi. Mhagama amesema hayo Septemba 27 2025 akiwa kwenye kampeni za kijiji kwa kijiji kunadi sera za Chama Cha Mapinduzi kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2025 -2030 katika kijiji cha Mborongo Kata ya Liganga, Songea Vijijini.
“Tunapokuja kuomba kura tunamaanisha, sisi CCM ndio ndugu zenu wa damu, Mborongo nitawashangaa, eti mtajenga imani ya chama cha upinzani, walikuwa na nafasi ya kuwaonyesha wao ni ndugu zenu wakati wa tabu, wanapokuja leo wakati wa raha, maji tumefanyia ’survey’, shule tumeshajenga, nyumba tunamalizia, zahanati na umeme tumeshaleta, haya yote tumeshayafanya, leo hii mkiwaamini nitawashangaa,” ameeleza Bi. Mhagama.
Bi. Mhagama amesema anatambua kero ya barabara iliyopo Mborongo na kusema kuwa endapo CCM itashinda, itaisimamia Serikali katika kukarabati barabara hiyo kwa gharama za Shilingi Milioni 120.