NA JOHN BUKUKU- PWANI
Mgombea wa Ubunge Jimbo la Kisarawe kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Dkt. Selemani Jafo, amewataka Watanzania kumpigia kura ya “ndiyo” kwa kishindo Mgombea wa Urais kupitia CCM, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 28, mkoani Pwani, Dkt. Jafo ameeleza kuwa Rais Samia amefanikisha maendeleo makubwa katika sekta mbalimbali nchini, ikiwemo elimu, afya, miundombinu na usafirishaji. Alisisitiza kuwa kazi hiyo kubwa ni kielelezo cha uongozi imara na dira ya maendeleo ya kweli kwa Watanzania.
Dkt. Jafo amebainisha kuwa kupitia diplomasia ya uchumi iliyoimarishwa na Rais Samia, mauzo ya bidhaa katika Soko la Afrika Mashariki yameongezeka na kufikia dola za Marekani bilioni 1.16, huku katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), mauzo yakiwa ni dola bilioni 2.9.
Akizungumzia maendeleo ndani ya Jimbo la Kisarawe, Dkt. Jafo amesema kuwa huduma ya umeme imesambazwa kwa asilimia 100, kutoka vijiji vinne tu vya awali hadi vijiji vyote 83 kufikiwa na umeme.
Kwa upande wa sekta ya afya, ameeleza kuwa jumla ya zahanati 27 zimejengwa, na Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe imeboreshwa kwa kiwango cha kutoa huduma za kibingwa. Aliongeza kuwa katika miaka mitano ijayo, lengo ni kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na zahanati ili kufanikisha kampeni ya “Kila Mtu Atibiwe Kwao”.
Kuhusu miundombinu, Dkt. Jafo amesema kuwa ujenzi wa barabara za lami unaendelea ili kuboresha usafiri na usafirishaji ndani ya jimbo hilo.
Katika sekta ya kilimo, Serikali inaendelea kujenga kiwanda cha kuchakata korosho pamoja na kuhamasisha ujenzi wa viwanda vingine ili kuongeza thamani ya mazao na kuchochea uchumi wa eneo hilo.
Sekta ya elimu pia imepewa kipaumbele, ambapo shule za msingi na sekondari zinaendelea kujengwa katika kila kata ili kuondoa changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya elimu.
Dkt. Jafo ametoa wito kwa wananchi wote wa Kisarawe na Tanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi na kumpigia kura Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ili aendelee kuwaletea Watanzania maendeleo endelevu.