NA JOHN BUKUKU- MTWARA
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali imejipanga kuhakikisha inatatua changamoto ya mafuriko yanayowakabili wakazi wa maeneo ya Chuno, Magomeni, Mtonya hadi Chikongola, mkoani Mtwara.
Akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika Septemba 26, 2025, katika Uwanja wa Saba Saba mjini Mtwara, Dkt. Samia alisema miradi ya kudhibiti mafuriko inaendelea kutekelezwa kwa lengo la kulinda maisha ya wananchi na mali zao, sambamba na kuimarisha miundombinu ya huduma muhimu.
Mbali na kudhibiti mafuriko, Dkt. Samia alisema miradi mbalimbali ya kimkakati imeendelea kuwanufaisha wananchi wa Mtwara na ukanda wa Kusini kwa ujumla. Alitaja kukamilika kwa kiwango kikubwa kwa miradi ya nishati katika wilaya za Newala na Masasi, jambo lililoongeza upatikanaji wa umeme.
Alibainisha kuwa Serikali inaendelea kuiwezesha TARURA na TANROADS kuboresha barabara za ndani zinazounganisha wilaya na makao makuu ya mkoa, ili barabara hizo zipitike mwaka mzima na baadhi kujengwa kwa kiwango cha lami.