Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan akikabidhi ilani ya uchaguzi kwa mgonbea ubunge Jimbo la Mtama Nape Nnauye katika muendelezo wa mikutano ya Kampeni za Uchaguzi kwa CCM, mkoani Lindi Septemba 24, 2025.
…………….
NA JOHN BUKUKU- MAMA LINDI
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea na kampeni za chama hicho Septemba 24, 2025 katika Jimbo la Mtama Mkoani Lindi. Amesema Serikali ya CCM itasogeza huduma za afya karibu na wananchi na kuanzisha mfumo mpya wa bima ya afya, huku akibainisha kuwa majaribio ya mfumo huo yataanza ndani ya siku mia za kwanza katika uongozi wake.
Dkt. Samia ameeleza kuwa msimu wa korosho unakaribia, na Serikali inajitahidi kuhakikisha bei ya zao hilo inabaki juu ili wananchi waweze kuwekeza sehemu ya mapato yao katika bima ya afya.
Katika sekta ya elimu, ameahidi kuwa VETA itafika mtaani kusaidia wananchi, huku akibainisha kuwa upatikanaji wa maji umepandishwa hadi asilimia 72 na miradi inayoendelea itafikia asilimia 90.
Vilevile, amesema Serikali inalenga kuhakikisha wananchi wote wanapata maji safi na salama, na kuendeleza utoaji wa nishati safi kwa wanawake kupitia umeme na gesi yenye ruzuku.
Katika sekta ya kilimo, Dkt. Samia amesema Serikali itaendelea na ruzuku ya pembejeo na matrekta, kusaidia wakulima kuzalisha mazao ya chakula na biashara kwa wingi.
Pia ameahidi kuboresha mabarabara ya ndani ya kilomita kumi katika mji wa Ruangwa, pamoja na ujenzi wa stendi na soko, huku akibainisha kuwa ataweka ushirikiano na madiwani wa halmashauri katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Awali akizungumza, mgombea ubunge Jimbo la Mtama, Nape Nnauye amesema kuwa jimbo hilo limepiga hatua kubwa za maendeleo. Amekumbusha kuwa umeme umefika vijiji vyote 93 vya jimbo, na vitongoji 332 tayari vimeunganishwa, huku kazi ikiendelea katika vitongoji vilivyobaki.
Amesema barabara nyingi zimejengwa na kupitiwa na matengenezo, madaraja yameimarishwa, na taa za barabarani na mitaani zimewekwa ili kuboresha usafirishaji na usalama wa wananchi.
Pia ameeleza kuwa sekta ya afya imeshuhudia maendeleo, huku hospitali ya wilaya, vituo vya afya na zahanati zikitoa huduma bora, na usafirishaji wa wagonjwa ukiwa umeboreshwa.
Nape Nnauye amebainisha mafanikio ya kiuchumi yaliyopatikana katika serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia, akisema kuwa zaidi ya Watanzania 150,000 wameajiriwa, mishahara imepanda, na ukusanyaji wa kodi umeimarishwa kutoka Trilioni 18 iliyokuwa ikikusanywa kwa mwaka na kufikia Trilioni 32 kwa make fedha zinazokusanywa zikitumika kwa maendeleo ya Mtama na maeneo jirani.
Mradi wa gesi Kusini unachangia uwezeshaji wa vijana, wanawake, na wenye ulemavu, huku miradi ya elimu na ujuzi ikilenga kuongeza fursa za ajira na kuimarisha maendeleo ya jamii. Amewataka wanamtama ifikapo Oktoba 29 wote waende kumpigia kura Dkt. Samia.