Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha NLD, Mhe. Doyo Hassan Doyo, akiwa mkoani Mara, wilaya ya Tarime, amewahakikishia wananchi kuwa endapo atachaguliwa kuwa Rais, atasitisha mikataba yote ya madini na kuipitia upya.
Mhe. Doyo amesema kuwa iwapo itabainika mikataba hiyo imeingiwa kwa njia ya rushwa au ufisadi, serikali yake itaiondoa na kuanzisha mikataba mipya yenye kuzingatia maslahi ya taifa. Aidha, ameongeza kuwa wananchi wazawa wa Tarime watapewa kipaumbele cha kwanza katika uwekezaji wa madini ili kuhakikisha rasilimali za taifa zinawanufaisha Watanzania wenyewe.
Akiwa Nyamongo, mkoa wa mara Mhe. Doyo alisisitiza kuwa haiwezekani eneo lenye mgodi mkubwa kama huo likakosa huduma bora za kijamii huku wageni wakiendelea kumiliki utajiri wa taifa. Alitolea mfano wa Saudi Arabia, akieleza jinsi wananchi wa nchi hiyo wanavyonufaika na huduma bora kutokana na mapato ya mafuta, na akasema wananchi wa Nyamongo hawapaswi kubaki wakitegemea kuendesha bodaboda pekee.
Kwa mujibu wa ahadi yake, endapo atachaguliwa kuwa Rais, serikali yake itahakikisha wananchi wa Mkoa wa Mara wanamilikishwa mgodi huo na kunufaika moja kwa moja na mapato yake.
Aidha, Mhe. Doyo amewaahidi wananchi wa Tarime kujengewa soko la kisasa. “Haiwezekani kwa namna Mkoa wenu wa Mara ulivyo na rasilimali nyingi, ikiwemo madini, wilaya ya Tarime ikakosa kuwa na soko la kisasa. Nitahakikisha tunajenga soko lenye hadhi na linalokidhi mahitaji ya wananchi,” amesema.
Mbali na hilo, Mhe. Doyo pia amesisitiza dhamira yake ya kuwekeza katika huduma za kijamii ikiwemo elimu, afya na miundombinu ya barabara, akieleza kuwa maendeleo ya wananchi ndiyo msingi wa ustawi wa taifa.
Kwa sasa, msafara wa mgombea huyo wa NLD upo Kanda ya Ziwa ukiendelea na mikutano yake ya kampeni, ambapo amekuwa akiwahimiza wananchi kuchagua uongozi unaojali maslahi ya wananchi na kulinda rasilimali za taifa kupitia Chama cha NLD.