NA JOHN BUKUKU- MASASI MTWARA
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea na kampeni za chama hicho Septemba 22, 2025 katika Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, ambapo amewahakikishia wananchi ujenzi wa barabara ya Mnivata–Newala–Masasi yenye urefu wa kilomita 100 kwa kiwango cha lami.
Dkt. Samia amesema ujenzi wa barabara hiyo ni miongoni mwa vipaumbele vitakavyotekelezwa na Serikali ya CCM katika awamu ijayo, ili kurahisisha usafiri na kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Mtwara na maeneo jirani.
Aidha, amesema sambamba na barabara hiyo, Serikali itaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa kongani za viwanda katika kila wilaya ya mkoa wa Mtwara, ikiwemo Masasi, ili kuongeza thamani ya mazao yanayolimwa na wananchi. Alibainisha kuwa kabla ya kufanikisha ujenzi wa viwanda hivyo, Serikali itahakikisha upatikanaji wa umeme wa kutosha kwa wananchi wote.
Akizungumza na wananchi na wakazi wa Masasi, Dkt. Samia aliongeza kuwa endapo CCM itapewa ridhaa na wananchi katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Serikali itaendelea kutoa huduma muhimu za kijamii, ikiwemo kukamilisha miradi ya maji, ujenzi na ukamilishaji wa zahanati pamoja na vituo vya afya, na kuhakikisha barabara zote za TARURA zinapitika mwaka mzima.
Vilevile, amebainisha kuwa Serikali itaendeleza miradi ya barabara, bandari na reli itakayounganisha Bandari ya Mtwara na Mbamba Bay, hatua ambayo itarahisisha zaidi shughuli za biashara na usafirishaji.
Dkt. Samia pia amewahakikishia wafanyabiashara wadogo, wakiwemo wamachinga, bodaboda, bajaji na mamalishe kwamba hawatasahaulika, kwani Serikali itaendelea kuwatafutia masoko na maeneo rasmi ya kufanyia biashara.
Aidha, amewahakikishia watu wenye ulemavu kuwa wataendelea kufaidika na asilimia mbili ya mikopo inayotolewa na Serikali kupitia halmashauri, ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.