Silivia Amandius
Bukoba, Kagera.
Kampuni ya Huduma za Meli Tanzania (TASHICO) imetoa shukrani kwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha ukamilishaji wa meli mpya ya MV Mwanza, mradi uliochukua zaidi ya miaka mitano kukamilika.
Mkurugenzi Mtendaji wa TASHICO, Ndg. Eric Hamiss, alisema meli hiyo itakuwa chachu ya ukuaji wa uchumi wa taifa na Kanda ya Ziwa kwa ujumla, kwa kuwa itaongeza fursa za biashara na kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo. Aidha, alibainisha kuwa meli hiyo itaendesha safari zake hadi Port Bell nchini Uganda, jambo litakaloimarisha uhusiano wa kibiashara na kikanda.
Meli hiyo imegharimu zaidi ya shilingi bilioni 126 na ina uwezo wa kubeba abiria 1,200 na mizigo yenye tani 400, huku ikikadiria kutumia kati ya saa 6 hadi 6 na nusu katika safari zake.
Mwakilishi wa mkandarasi kutoka kampuni ya Gas Entec Co. Ltd, Eng. Rayton Kwembe, alieleza kuwa meli hiyo imekamilika kwa asilimia 99, baada ya kuachwa kwa asilimia 30 kipindi cha uongozi wa Hayati John Pombe Magufuli.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kagera, Karim Amri, alisema ukamilishaji wa meli hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, huku wananchi mbalimbali akiwemo Anastazia Kweyamba na Amza Mzee wakieleza furaha yao kwa serikali kwa kufanikisha mradi huo ambao utaondoa adha ya usafiri na kuchochea biashara kwa urahisi zaidi.