MGOMBEA udiwani wa Kata ya Muriet kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kredo Kifukwe akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni.
……..
Happy Lazaro, Arusha .
Arusha .MGOMBEA udiwani wa Kata ya Muriet kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kredo Kifukwe, ameanza kampeni zake kwa kishindo, akiahidi kusimamia kikamilifu maendeleo ya kata hiyo na kuonya wakandarasi wazembe pamoja na taasisi zinazoshindwa kuwahudumia wananchi ipasavyo.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo uliofanyika Muriet ,Kifukwe aliahidi kuhakikisha analeta maendeleo katika kata hiyo kwa kushirikiana na viongozi mbalimbali ndani ya Chama cha mapinduzi.
Aidha katika uzinduzi huo mgombea udiwani huyo Kredo alikabidhiwa rungu la kimila kama ishara ya kuaminiwa na wananchi kuwa kiongozi wao.
Akihutubia mamia ya wananchi wa kata hiyo, amesema rungu hilo litakuwa alama ya kusimamia uwajibikaji na kuwashughulikia watendaji wazembe wanaoshindwa kuwatumikia wananchi.
“Barabara zetu ni mbovu sana. Nikiingia madarakani, wakandarasi wababaishaji wajipange, maji ya ugali hayaonjwi.”amesema Kredo .
“Nitahakikisha kila alivepewa dhamana ya kusimamia anawajibika ipasavyo katika kuhakikisha kata hii inakuwa na maendeleo na kuondokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili na tutahakikisha Muriet inashtua kwa maendeleo” amesema Kifukwe .
Akizungumza kuhusu maendeleo ya Taifa, Kifukwe amemsifu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa zilizotekelezwa chini ya uongozi wake, akibainisha kuwa mafanikio hayo yamewarahisishia wagombea wa CCM kuomba kura kwa wananchi.
Aidha alimnadi mgombea ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Paulo Makonda, akisema ni kiongozi mwenye uwezo mkubwa wa kiutendaji na ubunifu.
“Tumepewa Makonda Arusha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu. Ni kiongozi mwenye akili nyingi na ubunifu wa hali ya juu. Kufanya kazi na mbunge wa aina hiyo ni bahati kubwa, tunamwona kama lulu ya Arusha. Maendeleo lazima yajulikane,” amesema Kifukwe.
Aliyekuwa Diwani wa kata hiyo, Francis Mbise, alimhakikishia Kifukwe ushirikiano, akimpongeza kwa kuteuliwa kuwania nafasi hiyo na kukanusha madai kuwa ana kinyongo.
“Wanaosema nina kinyongo na Kredo wasitupotezee muda. Nimekonda kweli? Haya ni maneno ya wapambe. Nipo imara na moyo wangu ni mweupe. Nipo tayari kumpigia debe nyumba kwa nyumba ili ashinde kwa kishindo,” amesema Mbise
Kwa upande wake, Katibu wa Itikadi, Siasa na Uenezi wa CCM, Saipulani Ramsey, alimkabidhi rasmi Kifukwe ilani ya chama, akimtaka kuhakikisha anasimamia utekelezaji wake endapo atachaguliwa.
Ramsey amesisitiza kuwa mgombea huyo anatakiwa kupigania upatikanaji wa huduma za maji safi, uboreshaji wa miundombinu ya barabara, elimu, afya na mikopo ya kijamii ili wananchi wa Muriet wanufaike moja kwa moja na uongozi wake.
“Kila kitu kipo ndani ya ilani ya CCM,Kifukwe akishinda akihakikishe wananchi wananufaika na ilani hii, ndipo faida ya kukichagua chama cha Mapinduzi itakapoonekana,” amesema