NA JOHN BUKUKU
Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea kuwa kinara wa kampeni za kistaarabu kwa kuelekeza hoja zake katika sera, utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya make 2020–2025 na kueleza namna ambavyo CCM itakavyotekeleza Ilani ya mwaka 2025–2030.
Katika mikutano yake ya kampeni, Dkt. Samia amesisitiza umuhimu wa kudumisha amani na utulivu, akibainisha kuwa ni misingi inayokwenda sambamba na maendeleo ya taifa lolote duniani. Amesema kuwa bila amani, mipango ya maendeleo haiwezi kufanikishwa, kwani wananchi hukosa fursa ya kufikiri kwa utulivu na kutekeleza mawazo yao ya kiuchumi na kijamii.
Aidha, Rais Dkt. Samia ambaye Septemba 21, 2025 anatarajiwa kuhutubia mutano mwingine wa Kampeni kisiwani Pemba banda ya kumaliza mikutabo yake ya Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja na Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja amewakumbusha waandishi wa habari kuwa kalamu zao ni silaha kubwa ambazo zikitumika vizuri hujenga taifa, lakini zikitumika vibaya huweza kuvuruga mshikamano wa kitaifa. Vivyo hivyo, amesema ndimi za wanasiasa katika kipindi hiki cha kampeni ni silaha ambazo zikidhibitiwa vibaya zinaweza kuhatarisha amani na utulivu wa taifa.
Kauli yake imeenda sambamba na onyo la Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, ambayo imewataka wanasiasa kufuata sheria, kanuni na taratibu ili kuhakikisha kampeni zinafanyika kwa kistaarabu bila uchochezi wala lugha za mafarakano.
Viongozi wakuu wa Bara na Visiwani pia wamekuwa mstari wa mbele kusisitiza kuwa maendeleo yote yanayoshuhudiwa Tanzania leo ni matokeo ya amani na utulivu. Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewahi kusema: “Amani na utulivu vimeiwezesha Zanzibar kuwa kivutio cha uwekezaji na sekta ya utalii kustawi.”
Kwa upande wake, Dkt. Samia ameendelea kusisitiza: “Hakuna maendeleo bila amani. Tusipoilinda na kuithamini amani tuliyonayo, hatuwezi kufanikisha mipango yetu ya kitaifa.”
Miradi mikubwa ya maendeleo kama vile reli ya kisasa (SGR), bwawa la Julius Nyerere (JNHPP), barabara na viwanja vya ndege, pamoja na miradi ya uchumi wa bluu Zanzibar, imefanikishwa kwa sababu Watanzania wameendelea kulinda amani na mshikamano wa kitaifa.
Wito wa viongozi hao unabaki dhahiri: Amani na utulivu ndiyo nguzo za maendeleo. Kila Mtanzania anapaswa kushirikiana kuilinda, ili taifa liendelee kusonga mbele kwa mshikamano na kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika.