Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara, Mhandisi Mussa Natty (kulia) akimuelekeza jambo Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Barabara, Mhandisi Rashid Kalimbaga (kushoto), leo, Bodi hiyo ilipokagua kazi za matengenezo ya barabara katika Barabara ya Dodoma hadi Kitinku (Km 66.7) kwa fedha za Serikali kupitia Mfuko wa Barabara.
Wahandisi kutoka Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) wakifafanua jambo kwa wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara wakati Bodi hiyo ikikagua kazi za matengenezo ya barabara katika Barabara ya Dodoma hadi Kitinku (Km 66.7) zilizotekelezwa kwa fedha za Serikali kupitia Mfuko wa Barabara.
Wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo Mhandisi Mussa Natty (wa kwanza kulia), wakiangalia sehemu ya mtaro (m 450) uliojengwa katika barabara ya Dodoma hadi Kitinku (Km 66.7) katika eneo la Kizota,leo.
Matengenezo ya barabara yaliyohusisha uwekaji wa tabaka jipya la barabara kwa kutumia zege katika eneo la Nala Mizani katika barabara ya Dodoma hadi Kitinku (Km 66.7) uliotekelezwa kwa fedha za Serikali kupitia Mfuko wa Barabara.
Matengenezo ya barabara yaliyohusisha uwekaji wa tabaka jipya la barabara kwa lami katika eneo la Bahi, barabara ya Dodoma hadi Kitinku (Km 66.7) kwa fedha za Serikali kupitia Mfuko wa Barabara. (Picha na Baltazaar Mashaka)
NA BALTAZAR MASHAKA, DODOMA
WAJUMBE wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB),wamefanya ukaguzi katika mradi wa matengenezo ya barabara ya Dodoma hadi Kitinku yenye urefu wa kilomita 66.7, kujionea maendeleo ya kazi na kubaini maeneo yanayohitaji matengenezo zaidi.
Ziara hiyo imeongozwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mhandisi Mussa Natty, leo, ambapo wajumbe walipata fursa ya kutembelea sehemu mbalimbali za mradi huo unaotekelezwa kwa fedha za Serikali kupitia Mfuko wa Barabara.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, leo, Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Christina Nyamziga amesema kuwa matengenezo ya barabara hiyo yanagharimu shilingi milioni 911, na hadi sasa mradi umefikia hatua ya mwisho na uko chini ya uangalizi.
Amebainisha kuwa sehemu ya mradi huo inahusisha ujenzi wa mtaro wenye urefu wa mita 450 katika eneo la Kitinku, kwa ajili ya kulinda tabaka la barabara dhidi ya mmomonyoko na kupunguza athari za mafuriko kwa wakazi wa maeneo ya jirani.
Aidha, wajumbe wa Bodi hiyo pia, wamekagua ujenzi wa tabaka jipya la zege katika eneo la Nala Mizani, kazi inayolenga kuimarisha sehemu hiyo ya barabara kutokana na uzito mkubwa wa magari makubwa yanayopima uzito katika mizani hiyo.
Mwenyekiti wa Bodi, Mhandisi Natty, amesema kuwa wameshuhudia ukarabati wa barabara kwa kutumia lami mpya katika eneo la Bahi, ambapo mita 150 za barabara zilizokuwa zimeharibika zimetengenezwa ili kuboresha hali ya usafiri na kupunguza usumbufu kwa watumiaji wa barabara hiyo muhimu.
Hivyo, Bodi hiyo ya Mfuko wa Barabara, imeendelea na ziara zake za ukaguzi katika mikoa ya Singida, Manyara na Arusha, kufuatilia utekelezaji wa mradi mbalimbali ya barabara inayofadhiliwa na Serikali ya Awamu ya Sita kupitia mfuko huo, kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana namiundombonu ya barabara inaboresha kwa ufansi. sss