NA JOHN BUKUKU- MAKUNDUCHI
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametangaza mpango wa kuanzishwa kwa kituo maalum cha kumbukumbu na nyaraka za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kitakachokuwa rejeleo kwa vijana, wananchi na wageni wanaotaka kujifunza historia, maana na maendeleo ya Muungano.
Akihutubia mkutano mkubwa wa kampeni uliofanyika Kajengwa Makunduchi, Zanzibar, Dkt. Samia alisema tunu za umoja, amani na utulivu ndizo msingi wa maendeleo ya taifa, na ni jukumu la kila Mtanzania kuendelea kuzilinda.
“Tumedumisha umoja, amani na utulivu nchini. Hizi ndizo tunu za msingi katika maendeleo ya taifa letu. Kwa bidii zetu kubwa, niwahakikishie kuwa tutaendelea kulinda tunu za Muungano, umoja, utulivu na amani ya nchi yetu,” alisema Dkt. Samia.
Ameongeza kuwa tunu hizo zimeipa Tanzania utambulisho wa kipekee katika medani za kimataifa na kuifanya kuwa mbia muhimu wa kidiplomasia duniani, jambo linalothibitisha umuhimu wa kuenzi urithi wa Muungano.
Katika mkutano huo, Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, alisisitiza umuhimu wa kudumisha amani, mshikamano na maridhiano, akieleza kuwa ndio msingi wa maendeleo na mshikikiano wa kitaifa.