Na Meleka Kulwa-Dodoma
TUME ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Shirikisho la Vyama vya Ushirika (TFC), Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Konsotia ya Bima za Kilimo (TAIC), taasisi za kifedha na wadau wa bima ya zao la tumbaku, kwa kushirikiana na wakuu wa wilaya za Mkoa wa Tabora, wamekubaliana kuanza mara moja zoezi la usajili wa wakulima wa tumbaku kabla ya kuanza kwa msimu wa kilimo.
Makubaliano hayo yamefikiwa leo Septemba 17,2025 jijini Dodoma katika kikao kazi kilicholenga kuboresha huduma ya bima ya mazao na kuhakikisha wakulima wanalindwa dhidi ya majanga yanayoweza kuathiri uzalishaji.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Mrajis na Mtendaji Mkuu wa TCDC, Dkt. Benson Ndiege, amesema kuwa kupitia usajili huo, takwimu za wakulima zitakusanywa na kuhifadhiwa kwa matumizi ya kampuni za bima, taasisi za kifedha pamoja na wakulima wenyewe.
“Usajili huu tutaaanza kwa zao la tumbaku na baadaye utafuata kwenye mazao yote yanayosimamiwa na TCDC. Tutahakikisha unakamilika kwa haraka kabla ya kuanza kwa msimu wa kilimo cha tumbaku,” amesema Dkt. Ndiege.
Aidha ameongeza kuwa bima kwa wakulima kwa sasa ni jambo la lazima kwa kuwa inawalinda wanapokumbwa na majanga, huku akibainisha kuwa Serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha kila mkulima anakuwa na bima ya mazao.
“Kupitia ushirika, wakulima wataweza kupata huduma ya bima kwa urahisi zaidi, huku taasisi za kifedha na kampuni za bima zikihakikisha mfumo huo unakuwa endelevu.”amesema Dkt. Ndiege.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Dkt. Khamis Mkanachi, amesema kuwa usajili wa wakulima ni hatua muhimu na ya haraka, kwani bila ya zoezi hilo uhalali na utambuzi wa wakulima unabaki kuwa fumbo.
“Kukamilika kwa usajili huo kutasaidia kudhibiti vitendo vya utoroshaji wa tumbaku, kwa kuwa mkulima atakayekopeshwa na benki kupitia chama cha ushirika atalazimika kuuza tumbaku yake kupitia chama hicho na si vinginevyo.”amesema Dkt.Mkanachi
Wadau hao wameeleza kuwa bima ya mazao ni nguzo muhimu katika kulinda ustawi wa wakulima na kuongeza tija ya kilimo, jambo litakalosaidia sekta ya tumbaku kuchangia ipasavyo katika pato la taifa.