Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipowasili kwenye uwanja wa Nyota Nyeupe Kajengwa Makunduchi wilaya ya Kusini Unguja leo Septemba 17, 2025 visiwani Zanzibar ambapo amewaomba wananchi kumpigia kura za ndiyo katika uchaguzi mkuu wa Rais, Wanunge na Madiwani, utakaofanyika Oktoba 29, 2025 nchini kote.
Wanu Ameir Mgombea Ubunge Jimbo la Makunduchi akiwa tayari katika viwanja vya nyota Nyeupe wilaya ya Kusini Mkoa wa Kusini Unguja amezungumza machache kuhusu ujio wa Dkt. Samia.
…………..
NA JOHN BUKUKU- MAKUNDUCHI
Ujio wa Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mkoa wa Kusini Unguja Septemba 17, 2025, umeendelea kuibua hamasa kubwa miongoni mwa wananchi na viongozi wa maeneo hayo.
Katika mkutano huo unaofanyika Kajengwa, wananchi wameendelea kumiminika kwa wingi kumpokea Dkt. Samia, wakionesha ari na mapenzi makubwa ya kumkaribisha nyumbani.
Akizungumza kando ya mkutano huo kwa mahojiano maalum na mtandao wa Fullshangweblog, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Makunduchi, Wanu Ameir, alisema ujio wa Dkt. Samia ni faraja kubwa kwa wananchi wa Kusini, huku akiahidi kuendeleza alama iliyowekwa na kiongozi huyo katika jimbo hilo.
“Amelitumikia jimbo kwa uwezo wake mkubwa na ameacha alama. Naomba Mungu anisaidie na aniongoze, nawaahidi wana Makunduchi kufanya zaidi ya alivyofanya yeye,” alisema Wanu.
Aidha, Wanu alibainisha kuwa dhamira yake ni kufungua fursa za kiuchumi kwa vijana kupitia Uchumi wa Bluu, hususan katika sekta za uvuvi na utalii, pamoja na michezo ili kupanua wigo wa ajira na maendeleo.
Akigusia sekta ya elimu, alisema Makunduchi imepiga hatua kubwa, ambapo mabinti ambao awali walikuwa wakifanya vibaya sasa wamepanda hadi kufikia nafasi ya juu kitaifa. Pia alisisitiza mchango wa vyuo vya amali katika kuwanyanyua kielimu na kimaisha vijana waliokosa ufaulu.
Kwa ujumla, alisema ujio wa Dkt. Samia unazidi kuongeza matumaini mapya ya maendeleo kwa wananchi wa Kusini Unguja, huku akiwataka vijana kushirikiana naye ili kuhakikisha wananufaika na fursa hizo.