Na Meleka Kulwa- Dodoma
Mgombea udiwani wa Kata ya Kilimani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mussa Mkunda, leo Septemba 14, 2025 amezindua rasmi kampeni zake kwa kuomba ridhaa ya wananchi wa kata hiyo ili waweze kumpa nafasi ya kuwatumikia baada ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kilimani, Mkunda amesema changamoto kubwa inayowakabili wakazi wa kata hiyo, hususan katika mtaa wa Chinyoya, ni miundombinu mibovu ya maji taka, akiahidi kwamba endapo atachaguliwa, atashirikiana na serikali pamoja na wabunge kuhakikisha changamoto hiyo inatafutiwa suluhu ya kudumu.
“Wananchi wa Kilimani tunakabiliwa na kero kubwa ya miundombinu, hususan maji taka. Naomba ridhaa yenu ili kwa kushirikiana na Mbunge wa Dodoma mjini, Mheshimiwa Paschal Chinyele, tuhakikishe tunalitatua tatizo hili kwa miguu miwili,” amesema Mkunda.
Aidha, Mkunda amewaomba wananchi kumchagua yeye kwa nafasi ya udiwani, Chinyele kwa nafasi ya ubunge, na Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa urais,
Kwa upande wake, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Dodoma Mjini kupitia CCM, Mheshimiwa Paschal Chinyele, amesema kuwa serikali tayari imeanzisha mradi wa bomba kubwa la maji taka katika eneo la Swaswa ili kupunguza kero ya muda mrefu inayowakumba wananchi wa Kilimani.
Aidha, amebainisha kuwa, endapo CCM itapewa ridhaa kuendelea kuongoza jimbo hilo, wataomba serikali kuwapatia eneo la ujenzi wa Kituo cha Afya katika kata hiyo, hatua itakayowarahisishia wananchi kupata huduma muhimu za afya karibu bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.