NA JOHN BUKUKU- KIGOMA
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kigoma Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Clayton Revocatus Chipando maarufu kama Baba Levo, amempongeza na kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka zaidi ya trilioni 7 za uwekezaji wa miradi ya maendeleo katika Kigoma Mjini.
Akizungumza Septemba 14, 2025, wakati wa kampeni za CCM Kigoma Mjini, Baba Levo alisema fedha hizo zimewezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo maji, umeme na uwanja wa ndege wa kisasa.
“Dkt. Samia amepeleka zaidi ya trilioni 7 Kigoma Mjini, ikiwemo zaidi ya bilioni 7 kwa mradi wa maji. Zamani wananchi walitegemea majenereta kupata umeme, lakini sasa huduma ya gridi ya taifa imeleta mwanga mpya,” alisema Baba Levo.
Amesema ujenzi wa uwanja wa ndege wa Kigoma unaogharimu zaidi ya bilioni 36 ni hatua nyingine muhimu ya kufuta aibu ya zamani na kuipa heshima mpya Kigoma.
Aidha, Baba Levo alisema safari yake ya kisiasa imefungamana na maendeleo haya makubwa, huku akifananisha historia yake binafsi na ile ya Nelson Mandela wa Afrika Kusini, akieleza kuwa wananchi wamempa jina la “Mandela wa Kigoma.”
Ameongeza kuwa yuko tayari kujinyenyekeza kwa wananchi wake, kujibeba kama “chawa” au kusali kama “mchungaji,” mradi tu maendeleo yaliyosukumwa na serikali ya Dkt. Samia yafike kwa kila mmoja Kigoma Mjini.