Na Neema Mtuka , Nkasi
Rukwa: Wananchi wa kijiji cha Kalila kata ya Kabwe wilayani Nkasi Mkoani Rukwa wameiomba serikali inayoongozwa na chama cha mapinduzi kukamilisha ujenzi wa jengo la zahanati ya Kijiji hicho lililoshindwa kukamilika kwa kipindi kirefu.
Wakizungumza leo Septemba 14, 2025 katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika kijiji hicho baadhi ya wananchi akiwemo Ramadhani Masesa amesema ni aibu kubwa kuona mama mjamzito anajifungua njiani na kwenye mtumbwi jambo linaloshusha heshima na utu wa mtu.
Masesa amesema kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya miundombinu duni ya barabara pamoja na ukosefu wa huduma muhimu za afya , jambo linalochangia usumbufu mkubwa kwa wananchi hususani akina mama wajawazito na watoto.
“Shangazi yangu aliwahi kujifungulia kwenye mikono yangu tukiwa kwenye maji tumepanda boti ni aibu mimi sio mume wake nilitoa tu msaada kwa kweli tunawaomba wahusika watusaidie ni haki yetu kupata zahanati.”amesema Masesa.
Wananchi wamesisitiza kuwa licha ya juhudi mbalimbali zilizofanyika kwa kushirikiana na viongozi wa kijiji,bado maendeleo ya msingi kama barabara na zahanati yamekuwa yakisuasua kwa miaka mingi.
“Viongozi mbalimbali wakiwemo wa chama na serikali wamekuwa wakitoa ahadi zisizotekelezeka sisi sio wanyama wakina mama wanajifungulia kwenye maji na wakati mwingine mbele ya watoto wao hali hii haikubaliki kabisa” wamesema wananchi.
“Ukifika ziwani tayari mtoto amesha sogea inabidi uzae mtusaidie na sisi ni watanzania tunahitaji huduma kama wanavyopata wengine”Wamesisitiza.
Kijiji cha Kalila kipo Mwambao wa ziwa Tanganyika ili kupata huduma za afya hulazimika kupanda boti au mtumbwi ili kuokoa maisha yao na kupoteza muda mwingi kusaka huduma za afya.
Kwa upande wao viongozi wa chama cha mapinduzi (CCM) waliokuwepo katika mkutano huo akiwemo Katibu wa chama hicho wilaya ya Nkasi Anastasia Amos amekiri kupokea maombi ya wananchi na kuahidi kuyafanyia kazi mara baada ya chama kupata ridhaa ya kuongoza serikali.
Amesema makosa waliyoyafanya miaka mitano iliyopita wasirudie tena japo sio sababu ya wao kukosa zahanati lakini wakipata ridhaa ya kuongoza katika jimbo hilo la Nkasi kaskazini amewahakikishia wananchi hao kuwa wataondokana na changamoto hiyo.
Mgombea udiwani wa kata ya Kabwe ambaye aliingia madarakani miaka miwili iliyopita baada ya diwani aliyekuwepo kupoteza maisha Sebastian amewaomba wananchi ridhaa ili kuweza kuendelea pale alipoishia.
“Mimi na mgombea ubunge mkituchagua tutashirikiana kwa pamoja kuhakikisha kero hizo tunazitatua kwa pamoja.” Amesema diwani.
Akizungumza katika mkutano huo wakati wa kuomba kura kwa wananchi hao mgombea ubunge Jimbo la Nkasi kaskazini Salum Kazukamwe ameahidi kushughulika na changamoto hiyo na kufanya kuwa kipaumbele chake ni zahanati na barabara.
“Mkinipa ridhaa ya kuongoza Jimbo hili nitahakikisha huduma za afya zinatolewa kwa wananchi na mtaondokana na changamoto hiyo pamoja na miundombinu ya barabara.”amesema Kazukamwe .
“Kutokana na ukosefu wa miundombinu ya barabara mazao yenu yanaliwa na wanyama waharibifu wa mazao changamoto hii nimeipokea na nitashughulika nayo”.
Wananchi wa Kalila Wana matumaini kuwa kupitia uongozi imara wa chama cha mapinduzi matatizo yao ya muda mrefu yatapatiwa ufumbuzi wa kudumu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.