Afisa maendeleo ya jamii mkoa wa Arusha,Blandina Nnkini akizungumza katika semina ya viongozi wa dini na malwaigwanan iliyofanyika mjini hapa.\
Washiriki wa semina ya viongozi wa dini na malwaigwanan iliyolenga kujadili maswala mbalimbali ikiwemo haki za wanawake na watoto.
(Happy Lazaro).
………………………………………………………………………………………………………
Happy Lazaro,Arusha.
Tatizo la Ukatili dhidi ya wanawake na watoto miongoni mwa jamii huenda likapatiwa ufumbuzi wa kudumu Mara baada ya wizara ya katiba na sheria kuanza kuwapatia elimu viongozi wa dini na kimila ili waweze kuielimisha jamii kuhusu haki ya mwanamke na watoto.
Naibu katibu Mkuu wa wizara hiyo,Amon Mpanju amesema kuwa mafunzo hayo ya siku mbili yamelenga kutambua haki ya mwanamke,haki za binadamu na haki za watoto ,walemavu na makundi mengine kuweza kuthaminiwa .
Amesema kuwa viongozi wa dini na Mila wanaushawishi mkubwa katika jamii yao ,kuaminiwa hivyo hatua ya kupewa mafunzo hayo kutaisaidia serikali katika kutokomeza vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto vinavyozidi kushamiri miongoni mwa jamii.
“Tumieni majukwaa yenu ya dini na Mila kuisaidia serikali kutokomeza vitendo vya kikatili ,unyanyasaji dhidi ya wanawake ,watoto na walemavu ,najua mnamchango mkubwa sana kwa jamii myatumie mafunzo hayo kwenda kuielimisha jamii kwa kukemea hadharani” Amesema
Kwa upande wa viongozi wa dini akiwepo shehe Hussein Junje na Mchungaji wa kanisa la Maranatha kwa mrombo ,mchungaji Sadick Kinanga walisema kuwa,watahakikisha mafunzo hayo wanayopewa wanayatumia kwenda kutoa elimu juu ya haki za sheria dhidi ya wanawake na watoto na hatimaye kuweza kupunguza matukio ya ukatili wa kijinsia dhidi yao.
Hata hivyo walisema kuwa,wataweza kutumia nafasi zao kuhakikisha wanaelimisha jamii kupinga vita matukio hayo ya ukatili wa kijinsia kwani bado yanaonekana kushamiri katika jamii inayotuzunguka.
Naye Afisa maendeleo ya jamii mkoa wa Arusha ,Blandina Nkini alisema kuwa,tatizo la unyanyasaji na ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto mkoani hapa bado linaendelea kushika kasi,hivyo uwepo wa mafunzo hayo kwa viongozi hao itasaidia sana kuibadilisha jamii kutambua umuhimu wa kulinda na kuheshimu haki za wanawake, watoto na walemavu.
Mafunzo hayo ya siku mbili yanatolewa na wizara ya sheria na katiba kwa kushirikiana na mkoa wa Arusha ambapo yamewashirikisha viongozi hao kutoka mikoa ya Arusha na Manyara .