Vunjo, Kilimanjaro – Mgombea mwenza wa urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, ameendelea na mikutano yake ya kampeni kwa kishindo, ambapo leo amefanya mkutano mkubwa katika uwanja wa Polisi Himo, Jimbo la Vunjo, mkoani Kilimanjaro.
Akiwahutubia mamia ya wananchi waliojitokeza, Dkt. Nchimbi alitumia jukwaa hilo kuwatambulisha wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi kupitia CCM, akiwemo mgombea ubunge wa Jimbo la Vunjo, Ndugu Enock Zadock Koola pamoja na madiwani wa kata mbalimbali ndani ya jimbo hilo.
Katika hotuba yake, Dkt. Nchimbi alitoa wito kwa wananchi wa Vunjo na maeneo yote ya Kilimanjaro kumpigia kura kwa kishindo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na wabunge na madiwani wa CCM ifikapo Oktoba 29, 2025, akisema chama hicho kina rekodi ya utekelezaji mzuri wa ahadi zake.
Aliwapongeza wanachama wa CCM wa Jimbo la Vunjo kwa kuonyesha umoja na mshikamano baada ya mchakato wa ndani wa uteuzi, akisema ni jambo la kuigwa kitaifa. Dkt. Nchimbi pia alimpongeza Dkt. Charles Kimei, aliyewahi kuwa Mbunge wa Vunjo, kwa kuendelea kushiriki kikamilifu kwenye harakati za kisiasa na kumuunga mkono Rais Samia pamoja na wagombea wengine wa CCM.
Akichukua nafasi jukwaani, mgombea ubunge wa Jimbo la Vunjo kwa tiketi ya CCM, Ndugu Enock Zadock Koola, aliwasilisha maombi na ahadi zake kwa wananchi kwa msisitizo mkubwa juu ya changamoto ya barabara katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo. Alieleza kuwa baadhi ya barabara kama Chekereni–Mabogini–Kahe, Pofu–Mandaka–Kilema na Uchira–Kisomachi zimekuwa kero kwa wananchi na zinahitaji kufanyiwa kazi haraka.
Koola alieleza kuwa atahakikisha, endapo atapewa dhamana ya ubunge, atashirikiana na Serikali pamoja na taasisi husika kuhakikisha kuwa barabara hizo zinajengwa kwa viwango bora, ili kurahisisha usafiri wa watu na usafirishaji wa bidhaa, hasa kwa wakulima wa maeneo ya vijijini.
Aidha, alisisitiza kuwa uwepo wa miundombinu bora utachochea ukuaji wa uchumi wa ndani, kupunguza gharama za usafirishaji na kuongeza fursa kwa wananchi kupata huduma muhimu kama afya, elimu na masoko ya mazao yao kwa urahisi zaidi.
Koola alihitimisha kwa kusema kuwa yuko tayari kuwa kiongozi wa watu wote, atakayesikiliza na kushughulikia changamoto za wananchi kwa usawa. Aliahidi kuwa ofisi yake itakuwa wazi muda wote kwa wananchi bila ubaguzi, akisisitiza kuwa: “Ubunge si nafasi ya heshima tu, bali ni dhamana ya utumishi kwa wananchi wote wa Vunjo.”