NA JOHN BUKUKU- BUHIGWE KIGOMA
Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa Wilaya ya Buhigwe ni mji mkubwa na wa heshima kwa Taifa kwa sababu imetoa kiongozi mashuhuri, Makamu wa Rais wa sasa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, ambaye amehusika katika mipango mikubwa ya maendeleo ya nchi.
Akizungumza leo akiwa kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Buhigwe, Dkt. Samia alisema mchango wa Dkt. Mpango katika kupanga na kusimamia sera za maendeleo ya kitaifa ni jambo la kujivunia, na kwamba historia hiyo inaipa Buhigwe hadhi ya pekee.
“Buhigwe ni mji mkubwa kwa sababu umetupa kiongozi wetu Dkt. Mpango, ambaye amehusika kwenye mipango mikubwa ya kitaifa na kufanya mambo makubwa ya nchi. Hivyo mkiniamini tena kwa ridhaa yenu, tutaendelea kuing’arisha Buhigwe zaidi,” alisema Dkt. Samia.
Alibainisha kuwa serikali yake itaboresha miundombinu ya mji huo kwa kuweka taa za barabarani na kutandika lami kwenye barabara kuu na za ndani, hatua itakayosaidia kuinua biashara na shughuli za kiuchumi.
“Tutahakikisha vijana na akina mama wajasiriamali wanapata mazingira bora ya kufanya kazi saa 24. Tukiboresha barabara na kuweka taa, shughuli za biashara hazitalala, na kipato cha wananchi kitaongezeka,” alisisitiza Dkt. Samia.
Aidha, aliahidi kuendelea kusimamia miradi ya kijamii na kiuchumi mkoani Kigoma ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na fursa za maendeleo.