Na Sophia Kingimali
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas, ametoa rai kwa wadau wa maendeleo wakiwemo WWF kuendelea kushirikiana na Serikali ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kulinda hifadhi za misitu zilizopo nchini.
Wito huo ameutoa leo, Septemba 11, 2025 jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla ya upokeaji na uzinduzi wa vifaa vya usimamizi wa misitu na huduma za ugani na uenezi vilivyotolewa kupitia mradi wa mbinu za pamoja za upatikanaji wa nishati, mradi ambao umefadhiliwa na Umoja wa Ulaya kupitia WWF.
Amesema zipo juhudi mbalimbali ambazo Serikali imezifanya ili kuhakikisha rasilimali za misitu zinalindwa na kuhifadhiwa, ikiwemo kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa uhifadhi na madhara yatokanayo na uharibifu wa misitu.
“Serikali bado inawakaribisha WWF kuendelea kushirikiana nasi kupitia changamoto zilizopo, hasa zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi. Ili kuzishinda changamoto hizi, Serikali inahitaji ushirikiano wa wadau na tunawakaribisha sana,” amesema Dkt. Abbas.
Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi, Prof. Dos Santos Silayo, amesema wamejipanga kufanya kazi kwa umakini kuhakikisha maeneo ya hifadhi yanalindwa, huku wananchi wakipata nishati mbadala ambayo ni salama na endelevu na haitasababisha mabadiliko ya tabianchi.
“Karibu asilimia 75 ya kaya hapa nchini zinatumia nishati ya mimea. Sasa tunakwenda kuimarisha matumizi ya nishati safi na salama ili kulinda misitu yetu. Tunaendeleza pia kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia, ambayo kinara wake ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema Prof. Silayo.
Naye, Mkurugenzi wa WWF, Dkt. Amani Ngusaru, amesema wamekuwa wakisaidia shughuli za uhifadhi nchini kwa takribani miaka 30 sasa. Ameongeza kuwa wamejipanga kuendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha wanawajengea uwezo wadau wa uhifadhi ili maeneo ya hifadhi yawe salama.
Akizungumzia mradi huo, Savinus Kessy amesema mradi unakwenda kuleta mabadiliko chanya kwenye sekta ya nishati, huku ukizingatia zaidi uzalishaji.
Amesema mradi huo utaboresha miongozo ya usimamizi wa hifadhi za asili na kuongeza ufanisi wa taasisi za Serikali zinazohusika na sekta hiyo.
Mradi huo umegharimu zaidi ya shilingi bilioni moja, ambapo vifaa na vitendea kazi mbalimbali vimenunuliwa ikiwemo pikipiki, magari, boti ya mwendokasi, vifaa vya TEHAMA, jenereta pamoja na mifumo ya usimamizi na ufuatiliaji katika uhifadhi wa misitu.