Mgombea wa Nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan akikabidhi Ilani ya Uchaguzi kwa Mgombea Ubunge wa Chama hicho mara baada ya kuwahutubia wananchi wa Urambo katika muendelezo wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu kwa Chama hicho mkoani Tabora tarehe 11 Septemba, 2025.
………..
NA JOHN BUKUKU- URAMBO
MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, amewaahidi wakazi wa Mkoa wa Tabora kuwa, endapo chama hicho kitapata ridhaa ya kuongoza nchi, watakwenda kujenga shule 12 za msingi na sekondari.
Mgombea huyo alisema hayo Septemba 11, 2025 wilayani Urambo mkoani Tabora, wakati akiomba kura kwa wananchi na kueleza sera za CCM ambazo zitamuongoza katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Lakini katika kilimo tutajenga soko la mazao pamoja na skimu mbili za umwagiliaji, ambazo ni skimu za Uyogo na Izimbili.
“Jengine kwenye miundombinu, mama Sitta ameomba barabara hapa, sasa sina hakika kama barabara alizozitaja zimeingia zile alizoomba.
“Lakini kwenye Ilani yetu tumesema tutajenga barabara kwa kiwango cha lami; barabara za Emireti, Mnyonge na huko Usoke ambako aliomba Mama Sitta.
“Lakini pia kuna barabara ya Urambo–Jionee Mwenyewe–Ukwanga, barabara ya Igunguli–Milambo na hiyo nayo itakwenda kwa kiwango cha lami.
“Lakini barabara ya Urambo–Icheburanda–Kangeni nayo itajengwa kwa kiwango cha lami.
“Barabara nyengine ni Izimbili–Mabama, Tebena–Uwima, Usoke–Kalembena na Kingwa, zote zitajengwa kwa kiwango cha lami ndani ya miaka mitano inayokuja.
“Sasa sina hakika barabara aliyoiomba Mama Sitta, lakini jana nikiwa Igunga kuna barabara ilizungumzwa ambayo inatokea huko Kahama… Kwa hiyo nadhani tutaangalia ile iliyombwa Igunga na iliyombwa hapa na tuone tunaweza tukaziunganisha namna gani.
“Lakini jengine tutakalolifanya ni kujenga soko jipya katika mtaa wa St. Vicent pamoja na kuendeleza ujenzi wa vibanda katika stendi kuu ya mabasi.
Ndugu zangu, hayo ndiyo tuliyoyapanga lakini hatuna mwisho. Haja zinapotokea tutaendelea kuzitekeleza. Kama nilivyosema, masuala ya elimu, afya, maji na umeme ni ya kawaida, tutaendelea kuyafanyia kazi.
Awali, mgombea huyo alisema iwapo watapata ridhaa ya wananchi, serikali itawasogezea wakulima teknolojia mpya ya kukaushia zao la tumbaku.
Dk. Samia alisema teknolojia hiyo itakuwa mkombozi kwa wakulima hao kwani wamekuwa wakitumia kuni kukaushia zao hilo, hali inayoleta uharibifu wa misitu kutokana na ukataji miti kiholela.