Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Samweli Maneno akizungumza leo Septemba 11, 2025, wakati wa akifungua kikao kazi kati ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wahariri wa vyombo vya habari nchini, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mkemia Mkuu wa Serikali jijini Dodoma.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Bw. Rodney Mbuya akizungumza kwa niaba ya Msemaji wa Serikali wakati wa ufunguzi wa kikao kazi kati ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wahariri wa vyombo vya habari nchini, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mkemia Mkuu wa Serikali jijini Dodoma.
Mkuu wa Ktengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bi. Leila Mhanji akieleza lengo la kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari kuwa kujenga mahusiano ya karibu pamoja kuwafahamisha majukumu ya ofisi hiyo.
NA NOEL RUKANUGA, DODOMA
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imesema itaendelea kushirikiana na kutambua mchango wa vyombo vya habari nchini katika kuhakikisha umma unapata taarifa sahihi kuhusu haki na wajibu wa kila Mtanzania kupitia mifumo rasmi iliyowekwa na Serikali, jambo ambalo litawezesha utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa kwa ufanisi.
Akizungumza leo Septemba 11, 2025, wakati wa akifungua wa kikao kazi kati ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wahariri wa vyombo vya habari nchini, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mkemia Mkuu wa Serikali jijini Dodoma, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Samweli Maneno, amesema kuwa waandishi wa habari wana nafasi kubwa ya kuelimisha jamii katika nyanja mbalimbali ili kuchangia maendeleo ya Taifa.
Mhe. Maneno amesema kuwa katika kuhakikisha umma unapata uelewa mpana kuhusu sheria, ofisi hiyo kwa mwaka uliopita imefanikiwa kuandaa miswada 19 ya kisheria, na kutafsiri sheria 433 kati ya 446 zilizopo kutoka lugha ya Kiingereza kwenda Kiswahili.
“Lengo la kutafsiri sheria hizo ni kuwapa wananchi fursa ya kuzisoma na kuzielewa kwa urahisi ili kujenga utamaduni wa utii wa sheria bila shuruti. Kwa sasa zimesalia sheria 13 tu kukamilisha kazi hiyo, na tutaendelea kuwawezesha wananchi kufahamu sheria zaidi,” amesema Mhe. Maneno.
Ameeleza pia kuwa, ofisi hiyo imefanikisha kupitisha maazimio mawil iya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kufanya marekebisho ya sheria 446, ambazo tayari zimezinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na zimeanza kutumika rasmi.
Aidha, Mhe. Maneno amesema kuwa ofisi hiyo imekamilisha uchambuzi wa mikataba 3,446 ya kitaifa na kimataifa inayohusiana na ununuzi, ujenzi, ukarabati na utoaji wa huduma mbalimbali kwa jamii.
“Zaidi ya makubaliano ya awali (MoU) 700 yamefanyiwa mapitio na ofisi yetu ili kutoa ushauri wa kisheria kwa hatua zinazofuata,” ameongeza.
Amefafanua kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni chanzo sahihi na chenye mamlaka ya kikatiba katika masuala ya sheria, hivyo ni fursa muhimu kwa waandishi wa habari kutumia ushirikiano huo ili kutoa taarifa sahihi kuhusu namna Serikali inavyotekeleza masuala ya kisheria.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Bw. Rodney Mbuya, ameipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuandaa kikao kazi hicho muhimu ambacho kimewakutanisha wahariri kujifunza kuhusu utekelezaji wa majukumu ya ofisi hiyo.
Bw. Mbuya ametoa wito kwa vyombo vya habari na majukwaa ya habari nchini kuzingatia maadili, sheria na weledi hasa katika kipindi hiki ambacho Taifa linaelekea kwenye Uchaguzi.