Waziri wa Maji, Jumaa Hamidu Aweso akizungumza na mashabiki wa Simba katika kilele cha Tamasha la SIMBA DAY 2025 lililofanyika Septemba 10, 2025 katika uwanja wa Benjamini Mkapa, jijini Dar es Salaam
……………
Tamasha la SIMBA DAY 2025 limehitimishwa kwa mchezo wa kirafiki wa Kimataifa kati Wekundu wa Msimbazi Simba SC dhidi ya Gor Mahia ya Kenya
Mchezo huo wa kirafiki umefanyika leo Septemba 10, 2025 ambapo Simba SC imefanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Gor Mahia mchezo ambao umehitimisha sherehe za SIMBA DAY 2025 uliopigwa katika Uwanja wa Benjamini Mkapa.
Mbao ya Simba SC yamefungwa na Abdulrazak Hamza dakika ya sita ya mchezo na Steven Desse Mukwala dakika ya 65 na kufanikuwa kupata ushindi katika mchezo huo muhimu.
Katika mchezo huo Waziri wa Maji, Jumaa Hamidu Aweso, amemwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, kama Mgeni Rasmi katika kilele cha Wiki ya Simba.
Waziri Aweso ameungana na viongozi wa Simba SC pamoja na maelfu ya mashabiki waliomiminika kushuhudia burudani, utambulisho wa kikosi kipya cha msimu huu na shamrashamra zinazotambulisha heshima na hadhi ya klabu hiyo.
Simba Day, ambayo imekuwa ikifanyika kila mwaka, ni sehemu ya utamaduni wa klabu hiyo kongwe barani Afrika, ikileta pamoja wapenzi wa soka na burudani huku ikitoa taswira ya mshikamano mkubwa kati ya klabu na mashabiki wake.
Kilele cha maadhimisho ya mwaka huu kimeambatana na burudani kutoka kwa wasanii wakubwa, pamoja na matarajio makubwa ya mashabiki kuhusu kikosi kipya cha Simba kitakachoingia dimbani kwenye michuano ya ndani na kimataifa msimu wa 2025/26.