NA JOHN BUKUKU- IRAMBA SINGIDA
Vijana wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida wametakiwa kuchangamkia fursa zinazojitokeza mkoani humo ili waweze kupata kipato kitakachowasaidia kuendeleza maisha yao.
Maagizo hayo yametolewa na Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuwa kwenye mkutano wa kampeni mjini Iramba mkoani humo.
Amesema fursa zinapojitokeza ni vyema vijana wa maeneo husika wakachangamkia mapema ili zisichukuliwe na vijana kutoka mikoa jirani.
“Fursa zipo nyingi sana katika Wilaya ya Iramba. Mwaka 2023 nilipofanya ziara hapa niliahidi kuanzisha soko na tayari soko limeanzishwa Sherui, ambapo zaidi ya gramu milioni 1.5 zimeuzwa kwa thamani ya Shilingi bilioni 192 na fedha hizo zimeingia mikononi mwa wachimbaji,” amesema Dkt. Samia.
Aidha, ameeleza kuwa aliahidi kutoa kipaumbele kwa wachimbaji wadogo ambapo kulikuwa na maeneo yaliyokuwa yameshikiliwa bila kutumika. Serikali ilifuta leseni hizo na kugawa upya.
“Tumetoa leseni 32 kwa vikundi tisa ndani ya Wilaya ya Iramba pamoja na leseni nane za uchenjuaji wa madini ya dhahabu katika eneo la Sekenke. Yote haya ni kuhakikisha vijana wetu wanapata ajira za kutosha,” alisema Dkt. Samia.
Akizungumzia suala la nishati, Dkt. Samia alisema kuwa kwa Iramba kuna mradi wa umeme wa upepo wenye gharama ya zaidi ya Shilingi bilioni 80 na kwa sasa serikali inatafuta mbia ili kuanza uzalishaji wa umeme huo. Lengo ni kuongeza kiwango cha umeme ili maendeleo yajayo yakute umeme wa kutosha.
Aidha, aliongeza kuwa serikali inaendelea na utafiti wa mafuta na gesi, mradi ambao utaleta manufaa makubwa na kuvutia uwekezaji zaidi katika Wilaya ya Iramba, Igunga na maeneo ya Meatu. Alisema utafiti huo ukifanikiwa utachochea ajira nyingi zaidi.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba alisema tangu Uhuru kulikuwepo changamoto ya watoto kukaa chini shuleni kutokana na uhaba wa madawati, lakini sasa madawati ni mengi kiasi kwamba yanabaki. Pia madarasa yamejengwa ya kutosha na hivyo kusaidia watoto kusoma katika mazingira rafiki.
Aliongeza kuwa miundombinu mbalimbali imetekelezwa vizuri katika Wilaya ya Iramba ikiwemo maji, umeme na barabara.
“Wananchi hawa watakwenda kukuchagua kwa kishindo kwani umekuwa mwaminifu katika kutekeleza ahadi zote ulizozitoa katika Wilaya ya Iramba,” alisema Dkt. Nchemba.
Kwa upande wake, Jesca Kishoa alisema Mgombea Urais huyo amewafanyia mambo mengi mazuri ikiwemo sekta ya elimu, hivyo wanasubiri kupiga kura za ndiyo ili azidi kuwaletea maendeleo.
“Ulituletea Shilingi bilioni 14.2 kwa ajili ya sekta ya elimu ambapo tulijenga madarasa na kukarabati miundombinu mbalimbali ya elimu, pamoja na mambo mengine mengi mazuri uliyotufanyia. Hivyo Oktoba ni kutiki tu,” alisema Kishoa