Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwasalimia wananchi wa Mlowa katika Jimbo la Mvumi, mkoani Dodoma, wakati wa muendelezo wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu tarehe 07 Septemba, 2025.
……………..
NA JOHN BUKUKU- MLOWA-MVUMI
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema chama hicho hakina kawaida ya kudharau changamoto hata ndogo, bali kimejipanga kuzishughulikia ipasavyo ili zisigeuke kuwa kero kubwa kwa wananchi.
Akihutubia mamia ya wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika Mlowa, Jimbo la Mvumi mkoani Dodoma, Dkt. Samia alisema:
“Kama misumari imelala, hii miba iliyochomoza lazima tuishughulikie ipasavyo. Waswahili wanasema anayedharau mwiba ukimchoma huota tende. Sisi CCM hatutaki kudharau mwiba.”
Aliongeza kuwa wingi wa wananchi wanaojitokeza katika mikutano ya kampeni ni kielelezo cha imani kubwa kwa Serikali ya CCM kutokana na kazi iliyotekelezwa.
“La pili, wana-CCM wameridhishwa na kazi iliyofanyika na ndiyo maana kila tunapokanyaga kuna utitiri wa watu wanakuja kutusikiliza. Watu ni wengi sana kwa sababu wameridhishwa na kazi ambayo Serikali ya Chama Cha Mapinduzi imefanya, na hilo ndiyo jibu kubwa kuliko yote,” alisema huku akishangiliwa.
Katika mkutano huo, Mbunge wa Jimbo la Mtera, Livingstone Lusinde, alibainisha kuwa baadhi ya watu wanasema Dkt. Samia anatumia nguvu kubwa katika kampeni zake, lakini akifananisha hali hiyo na mapambano dhidi ya nyoka.
“Unapokutana na nyoka mkubwa ukampiga kwa fimbo kubwa na kumuua, akitokea nyoka mdogo utatumia ile ile fimbo kubwa kumuua,” alisema Lusinde, akisisitiza umuhimu wa CCM kupambana kwa nguvu sawa katika ngazi zote.
Aidha, Dkt. Samia alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi wa Mvumi kuendelea kuiamini CCM na kuwapigia kura wagombea wake wote.
“Sasa nimesimama hapa kuomba kura. Sina wasiwasi wowote na Mkoa wa Dodoma, sina kabisa. Lakini uungwana unapokuwa na shida ni kwenda kuomba kwa heshima, si ndiyo? Kwa hiyo nami kwa heshima na taadhima wanamvumi, nimesimama hapa kuomba kura nikimuombea kura mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, ambaye ndiyo huyu mama aliyesimama. Pia naomba kura kwa mgombea ubunge Livingstone Lusinde na madiwani wote wa CCM,” alisema Dkt. Samia.
Wananchi wa Mlowa walimshangilia kwa wingi na kuahidi kumpa kura za kishindo yeye pamoja na wagombea wote wa CCM katika uchaguzi ujao.