Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza katika. mkutano wa Kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa Tandale mjini Tukuyu wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya Septemba 05, 2025.
………..
NA JOHN BUKUKU- RUNGWE
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewahakikishia wakulima wa wilaya ya Rungwe na mikoa jirani kuwa Serikali itaendelea kulipa kipaumbele zao la parachichi kwa kulifanya kuwa zao la kimkakati lenye kuongeza kipato cha mkulima mmoja mmoja na kuchochea uchumi wa taifa.
Akihutubia wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Tandale, mjini Tukuyu wilayani Rungwe, Dkt. Samia aliwaomba kura za ndiyo ili aendelee kutekeleza mipango ya Serikali kwa manufaa ya wakulima.
Dkt. Samia alisema Serikali itaajiri maafisa ugani maalumu kwa ajili ya zao la parachichi na kuwapanga kwenye maeneo yanayolima zao hilo ili kusaidia wakulima kuongeza tija.
Maafisa hao watakuwa na jukumu la kupima udongo, kutoa elimu ya kilimo bora, kushauri pembejeo na mbolea bora pamoja na huduma nyingine muhimu za ugani.
Amesema Serikali itajenga vituo 50 vya kuhifadhia parachichi na mbogamboga, ambapo viwili vitakuwa wilayani Rungwe.
Vituo hivyo vitakuwa na teknolojia ya baridi ili kuhifadhi parachichi kwa miezi mitatu, hatua itakayosaidia wakulima kusubiri soko la kimataifa liwe na bei nzuri badala ya kuuza kwa hasara.
Kupitia mpango wa Jenga Kesho iliyo Bora (BBT), vijana wa Rungwe watajengewa viwanda vidogovidogo vya kuongeza thamani ya parachichi.
Kwa mazao yanayoharibika haraka, viwanda hivyo vitazalisha bidhaa mbadala kama mafuta, chakula cha mifugo na bidhaa nyingine, jambo litakaloongeza ajira na kipato cha vijana.
Dkt. Samia amesema Serikali imetoa miche ya parachichi milioni moja bure kwa wakulima wa Rungwe na mikoa mingine ili kupanua wigo wa uzalishaji.
Hii inalenga kuwahamasisha wakulima wapya kuingia kwenye kilimo cha parachichi.
Ameeleza kuwa ruzuku ya Serikali itaendelea kwenye zao la parachichi kupitia upatikanaji wa mbolea na dawa za kupulizia.
Tayari Serikali imenunua dawa ya kuanzia aina ya COPERSALPHET yenye thamani ya shilingi milioni mbili ili kudhibiti magonjwa na kuimarisha ubora wa mazao yanayokwenda sokoni.
Kwa ujumla, Dkt. Samia aliwaomba wananchi wa Rungwe wampe kura za ndiyo ili aendelee kutekeleza sera na mipango hiyo, akibainisha kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha parachichi linakuwa zao la kibiashara lenye ushindani wa kimataifa.