Makamu wa Rais wa Zimbavwe, Mheshimiwa Kanali Mstaafu Kembo Mohadi ameendelea kuishukuru Tanzania kwa mchango mkubwa iliyotoa kuzikomboa nchi za Kusini mwa Afrika ikiwemo Zimbabwe.
Kanali Mohadi ametoa shukrani hizo Agosti 31, 2025 alipotembelea Chuo cha Wazazi cha Kilimo kilichopo Kaole mjini Bagamoyo ambacho awali kilikuwa Kambi ya wapigania uhuru.
“Asante sana kwa kutukomboa, asante sana kwa kutupatia ardhi, asante sana kwa kutuhifadhi. Huu ni ukarimu mkubwa ambao Tanzania mliuonesha bila kujali madhara yake kutoka kwa wakoloni,” alisema Kanali Mstaafu Mohadi.
Hata hivyo, Makamu wa Rais Mohadi ametahadharisha kuwa, licha ya Afrika kupata uhuru wa kisiasa lakini uhuru wa kiuchumi bado haujapatikana na ili kufikiwa lazima Afrika iungane kutetea rasilimali zake.
Mheshimiwa Mohadi alisema ziara yake katika chuo hicho imelenga kukumbuka hatua kwa hatua, njia walizopitia wapigania uhuru na magumu waliyokumbana nayo ili iwe somo hasa kwa wale ambao hawakuwepo kipindi hicho. Kambi hiyo waliwahi kuishi Rais wa sasa wa Zimbabwe, Mheshimiwa Emmerson Mnangagwa, Marais Wastaafu wa Msumbiji, Hayati Samora Machel na Mheshimiwa Joaquim Chissano ambao aliwataja kama moja ya nguzo katika viongozi wa Afrika.
Naye, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Mhe.Fadhil Maganya ameutaja ukarimu ulioneshwa na Rais wa Zimbabwe, Mhe. Mnangagwa kwa kukipa zawadi ya Dola za Marekani 110,000 Chuo hicho ambazo zimetumika kukarabati mabweni, madarasa, cliniki ya mifugo na miundombinu mingine kuwa ni kielelezo cha uhusiano imara kati ya Tanzania na Zimbabwe, CCM na ZANU-PF, vyama tawala vilivyopigania uhuru wa nchi hizo.
Wakati wa kutembelea chuo hicho, Mheshimiwa Mohadi aliongozana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi na kupokewa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Shaibu Ndemanga, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM na viongozi wa chuo hicho wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi na Mkuu wa Chuo.