NA JOHN BUKUKU, KIBAIGWA KONGWA
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Taifa na Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM Dkt Samia Suluhu Hassan ameahidi kuleta mabadiliko makubwa kwa wana Kibaigwa wilayani Kongwa
Dkt. Samia ameyasema hayo wakati akizungumza na maelfu ya wananchi waliojitikeza kwenye mkutano wake wa kampeni uliofanyika mjini Kibaigwa Wilayani Kongwa mkoa wa Dodoma
“Nilipopita hapa Julai 2021 nilikutana na wanakongwa wakiwa na mbunge wao marehemu na wakati ule kulikuwa na changamoto kadhaa ambazo nilielezwa na niliahidi kwamba nitaendelea kuleta fedha kwa ajili ya maendeleo ya jimbo hili la Kongwa” amesema
Ameongeza kuwa “Tulifanya hivyo na matokeo yake sasa ni dhahiri na ni mashuhuda na mmemsikia mgombea ubunge wa jimbo la Kongwa ameyataja machache sana”
Aidha akizungumzia sekta ya elimu Dkt Samia amesema “Mbali na ujenzi wa shule za sekondari na msingi tumekamilisha ujenzi wa chuo cha Veta kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 2 na kuwawezesha vijana wetu kupata ujuzi wa fani mbalimbali ili waweze kujiajiri na kuajiriwa”
“Pamoja na kuendelea na elimu bila malipo tumeongeza shule za sekondari na kwa sasa ni 45 na kuwezesha wanafunzi wengi zaidi kupata nafasi” amesema
Ameongeza kuwa pia “Tumeboresha huduma za afya kwa kuongeza vituo vipya 14 na sasa kuna jumla ya vituo 73 hii ni pamoja na kuongeza majengo 14 mapya ikiwemo jengo la huduma za dharura katika hospitali ya wilaya yenye thamani ya shilingi bilioni 4.5 pamoja na vifaa tiba vya kisasa”
“Kituo cha afya cha Kibaigwa hapa sasa kinatoa huduma mpaka za Xray na tumeleta mashine ya Xray mpya na ya kisasa huduma ambazo wananchi wa Kibaigwa walikuwa wazifuate Dodoma mjini sasa zinapatikana hapa Kibaigwa” amesema
Dkt Samia amesema “Vijiji vyote vya Kongwa vina umeme na tunaendelea na kazi ya kusambaza umeme kwenye vitongoji kwenye taasisi na majumbani kwa watu”
“Nilipopita hapa mwaka juzi 2021 niliahidi kuwa tutajenga eneo la maegesho ya malori na nafurahi kuona ujenzi huo unaendelea na nitahakikisha unakamilika” amesema