Wanafunzi wa shule za Msingi Nyanza na Nyanza English Medium, wakimsikiliza Ofisa wa Polisi, Kata ya Mirongo, Mkaguzi Fatuma Mpinga, leo, wakati akitoa elimu ya madhara ya dawa za kulevya.
Ofisa wa Polisi Kata wa Mirongo, Mkaguzi Fatuma Mpinga, akitoa elimu ya madhara ya matumzi ya dawa za kulevya, akiwa amezungukwa na wanafunzi, leo.
Wanafunzi akiwemo mmoja wa walimu wakifuatilia kwa makini elimu ya madhara ya dawa za kulevya, leo ikitolewa na Mkaguzi wa Polisi, Fatuma Mpinga. Picha na Baltazar Mashaka
…………….
NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
KATIKA jitihada za kupambana na ongezeko la matumizi ya dawa za kulevya miongoni mwa watoto na vijana, Jeshi la Polisi limetoa elimu kwa wanafunzi wa shule za msingi mkoani Mwanza, kuhusu madhara ya uraibu huo hatari kwa afya, jamii na taifa kwa ujumla.
Mkaguzi wa Polisi wa Kata ya Mirongo,Mkaguzi Fatuma Mpinga, ametoa elimu hiyo katika Shule za Msingi Nyanza “B” na Nyanza English Medium, zilizopo Wilaya ya Nyamagana, ambapo alikutana na wanafunzi kwa nyakati tofauti kuwafundisha kuhusu athari kubwa za matumizi ya dawa za kulevya pamoja na mbinu za kujikinga na vishawishi vya kuingia katika mtego huo.
Katika mafunzo hayo yaliyotolewa leo, Insp. Fatuma amewaeleza wanafunzi hao kuwa dawa za kulevya zinaharibu afya ya akili na mwili wa mtumiaji.
Amesema kuwa, baadhi ya watumiaji wa dawa hizo, hukumbwa na matatizo ya afya ya akili, kupoteza kumbukumbu, nguvu za mwili kushuka, na wengine hukumbwa na magonjwa sugu ya moyo, ini na mapafu.
“Matumizi ya dawa za kulevya huathiri ukuaji wa ubongo na uwezo wa mtu kufikiri kwa haraka. Mtoto anaweza kuacha kabisa kusoma, kupoteza mwelekeo wa maisha na kuishia kuwa ombaomba au mhalifu mitaani,” amesema Insp. Fatuma.
Amewaeleza wanafunzi hao kuwa, zaidi ya madhara ya kiafya, uraibu wa dawa za kulevya hugharimu familia upendo na amani, ambapo vijana wengi wanaojiingiza kwenye matumiz ya dawa hizo, huiba nyumbani, hupoteza heshima kwa wazazi na hatimaye kuvunja mshikamano wa kifamilia.
“Watoto wanaotumia dawa za kulevya huacha kusikiliza wazazi na walimu, huchangia ongezeko la uhalifu mitaani na huweza kusababisha hata mauaji au madhara makubwa kwa wengine,” amesema Insp.Fatuma.
Mkaguzi huo wa Polisi, amewataka wanafunzi kuwa na ujasiri wa kusema hapana kwa yeyote atakayewalaghai au kuwashawishi kutumia dawa hizo, akisisitiza umuhimu wa kutoa taarifa mapema kwa mamlaka husika.
“Taarifa zenu ni muhimu sana, msisite kusema mnapoona au kushudia vitendo vya ushawishi vinavyohusiana na dawa za kulevya, mnapaswa kuzifikisha kwa wazazi, walimu au polisi. Hii itasaidia kuwaokoa wengine pia,” amesema kwa msisitizo.
Aidha, amewataka wazazi na walezi kuchukua jukumu la kuwa karibu na watoto wao, kuwasikiliza na kuwajengea msingi mzuri wa maadili na mawasiliano, ili kuwaepusha na makundi potofu mitaani yanayoweza kuwaharibu kimaadili.
“Elimu ya kupambana na dawa za kulevya haipaswi kuishia darasani tu, wazazi na jamii kwa ujumla mnatakiwa kushirikiana na vyombo vya dola kuwajenga vijana wetu kwa maadili na nidhamu,” ameeleza Insp. Fatuma.
Mkazi wa Nyamagana, Tausi Shaaban, amesema elimu hiyo ni sehemu ya jitihada za serikali kupitia Jeshi la Polisi kuhakikisha taifa linalinda rasilimali yake muhimu (vijana), kwa kuanzia katika shule za msingi, ni hatua ya msingi kuzuia mzizi wa tatizo kabla haujakomaa, ili kujenga jamii yenye afya, maadili na tija kwa maendeleo ya taifa.
Naye Joseph Kamuzora, ameeleza kuwa, kuimarisha ushirikiano kati ya shule, familia na vyombo vya dola, tatizo la dawa za kulevya linaweza kupunguzwa kwa kiasi kikubwa, na taifa likapata kizazi chenye afya bora, akili timamu na uwezo wa kujenga uchumi wa kisasa.