Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
Mgombea udiwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kata ya Pangani, John Katele, amerudisha fomu ya kugombea na kuahidi endapo atachaguliwa katika Uchaguzi Mkuu  Oktoba mwaka huu, atahakikisha anasimamia utekelezaji wa mradi wa maji unaoendelea ili kuondoa kero ya muda mrefu ya upatikanaji wa maji safi kwa wananchi.
Akizungumza mara baada ya kurudisha fomu hiyo, Katele alisema atashirikiana kwa karibu na viongozi wa serikali, chama pamoja na watendaji wa kata kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa kasi na kwa viwango vinavyostahili.
“Katika vipaumbele vyangu, kero ya maji ndiyo ya kwanza,Nitahakikisha inapata suluhisho la kudumu,” alisema Katele.
Aidha, aliahidi kushughulikia upatikanaji wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa makundi maalum wakiwemo wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, ili kuwawezesha kiuchumi na kuinua maisha yao.
Katele aliongeza kuwa masuala mengine atakayoyapa kipaumbele ni pamoja na kuboresha miundombinu ya barabara, kujenga mahusiano bora kati ya chama na serikali, na kuhakikisha kunakuwepo na umoja na usalama ndani ya kata hiyo.
Aliwaomba wananchi na wanachama wa CCM kuendelea kukiamini chama hicho kwa kukipa ushindi mkubwa ifikapo Oktoba 29, 2025.