Na Silivia Amandius.
Ngara, Kagera
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Ngara kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dotto Bahemu, amewaomba wanachama wa chama hicho kuvunja makundi na kuungana kwa ajili ya kuhakikisha ushindi wa kishindo kwa CCM kuanzia ngazi ya Urais hadi udiwani. Bahemu amesema hayo leo Agosti 26, 2025 mara baada ya kuchukua fomu ya uteuzi katika ofisi ya msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Ngara.
Bahemu amesema kuwa kipindi cha kura za maoni kimekwisha, na sasa ni muda wa kusahau makundi ya ndani ya chama na kushirikiana kwa pamoja katika kuhakikisha chama kinashinda kwa kishindo. Ameahidi kushirikiana na kila mwanachama, akiwemo wale waliokuwa hawamuungi mkono awali, ili kuhakikisha malengo ya chama yanatimia.
Amesisitiza kuwa atawafuata na kuzungumza na wanachama waliokuwa upande tofauti wakati wa kura za maoni ili kuelewa changamoto zao na kuwaunganisha kwa ajili ya mafanikio ya chama. Pia amewaomba wananchi wa Ngara kudumisha amani wakati wote wa kipindi cha uchaguzi.
Kwa upande wake, Msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Ngara, Constantino Msemwa, amesema Bahemu ametimiza vigezo vyote na kukabidhiwa fomu rasmi ya uteuzi. Naye aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Ndaisaba Ruholo, ameahidi kumpa ushirikiano kamili Bahemu na kuwaomba wananchi wampe mgombea huyo sapoti ili CCM iendelee kushika hatamu.