Na Sophia Kingimali
Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa umezindua mfumo wa kisasa unaoitwa Kijani Ilani Chatbot, ambao utarahisisha kwa vijana kupata taarifa za utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020–2025 pamoja na ahadi za chama kwa kipindi cha mwaka 2025–2030, kupitia simu zao za mkononi wakiwa popote.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mfumo huo uliofanyika jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Mohammed Ali Kawaida (MCC), alisema kuwa lengo la Kijani Ilani Chatbot ni kuwaonyesha vijana wa Kitanzania na Watanzania kwa ujumla namna Chama Cha Mapinduzi kinavyotekeleza ahadi zake ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Kijani Ilani Chatbot itatuonyesha ilani yetu ya uchaguzi ya mwaka 2025–2030 na mambo ambayo imeahidi, hususan kwa upande wa vijana wa Kitanzania,” alisema Kawaida.
Aidha, aliwasihi vijana kutumia kikamilifu mfumo huo kupata majibu ya maswali kuhusu ilani na utekelezaji wake ili kuongeza uelewa na kuepuka upotoshaji.
“Twendeni tukautumie mfumo huu ili kuondoa upotoshaji unaofanywa na watu wasiokuwa na mapenzi mema na taifa letu, kwa kuwaeleza na kuwaonyesha Watanzania ukweli,” aliongeza Kawaida.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Halid Mwinyi, alisema mfumo huo utawezesha mawasiliano ya moja kwa moja ambapo watumiaji watauliza maswali na kupata majibu kwa haraka na kwa njia rahisi, sambamba na kujifunza kuhusu uchaguzi na ilani ya CCM.
Ameongeza kuwa mfumo huo utatoa taarifa sahihi na za kidijitali kuhusu ilani ya CCM, miradi ya maendeleo na namna jamii, hususan vijana, inavyonufaika.
“Mifumo ya kidijitali itawawezesha vijana kuuliza maswali na kupata majibu papo kwa papo kupitia Kijani Ilani Chatbot. Pia itaongeza uelewa wao kuhusu nafasi ya vijana katika maendeleo ya taifa na ushiriki wa kisiasa, huku ikikuza matumizi ya teknolojia ya akili mnemba katika elimu ya siasa na utawala bora,” alisema Mwinyi.