Arusha, 23–26 Agosti 2025
Serikali imetambua mchango mkubwa wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) katika kuunga mkono juhudi za maendeleo ya taifa na kuikabidhi cheti cha heshima kwa kutambua nafasi yake kama mdhamini wa Mkutano wa Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Serikali uliofanyika jijini Arusha.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, ambaye alikuwa mgeni rasmi wa kufunga mkutano huo, alimkabidhi cheti hicho Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Mstaafu Jenerali Venance Mabeyo na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NCAA, mbele ya viongozi mbalimbali wa serikali na taasisi.
Dkt. Biteko alisema hatua hiyo ni ishara ya kuthamini juhudi za taasisi zinazoshirikiana na serikali katika kuimarisha mifumo ya usimamizi, uwajibikaji na ufanisi wa mashirika ya umma. “Serikali inatarajia taasisi zote kuendeleza mshikamano huu, kuongeza tija na kusimamia miradi ya maendeleo kwa weledi na ufanisi,” alisema.
Kwa upande wake, Jenerali Mabeyo aliishukuru serikali kwa heshima hiyo na kusisitiza kwamba NCAA itaendelea kushirikiana na wadau wote kulinda na kuhifadhi rasilimali za taifa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Mkutano huo wa siku nne pia umeazimia kuanzisha mfumo wa pamoja wa ufuatiliaji na tathmini ya utendaji wa taasisi za umma na kupendekeza marekebisho ya sera na sheria ili kuimarisha utawala bora na uwajibikaji.